Islamabad. Watu kadha wakamatwa katika msako unaoendelea nchini Pakistan.
21 Julai 2005Majeshi ya usalama ya Pakistan yamewakamata zaidi ya watuhumiwa 200, Waislamu wenye imani kali katika msako unaoendelea.
Kuna taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa kijana mmoja wa Kiislamu raia wa Uingereza ambaye anaaminiwa kuwa anatafutwa kwa kuhusika na mashambulio ya mabomu dhidi ya mji wa London hapo Julai 7 ni mmoja kati ya watu waliotiwa mbaroni.
Pakistan imekuwa chini ya mbinyo ili kuchukua hatua dhidi ya Uislamu wa imani kali tangu ilipotokea kuwa watu watatu waliohusika katika mashambulizi hayo ya kujitoa muhanga mjini London walikuwa Waingereza wenye asili ya Pakistan. Watu hao watatu pia walitembelea Pakistan katika muda wa mwaka mmoja uliopita. Misako na ukamataji huo unakuja baada ya rais Pervez Musharraf kutoa amri ya kufanyika msako mpya dhidi ya wanaharakati.