ISLAMABAD : Pakistan yasitisha shughuli za uokozi
14 Oktoba 2005Serikali ya Pakistan imekamilisha juhudi zake za kuwatafuta watu walionusurika kutokana na tetemeko la ardhi la Jumamosi iliopita na hivi sasa itaelekeza zaidi juhudi hizo katika kutafuta maiti na kujenga upya maeneo yalioangamizwa.
Hatua hiyo inakuja baada ya Umoja wa Mataifa kuelezea wasi wasi wake juu ya hali mbaya inayowakabili makumi ya maelfu ya Wapakistani ambao wamekuwa wakilala nje na kupigwa na baridi kutokana na nyumba zao kuangamizwa na tetemeko hilo la ardhi.
Mratibu mkuu wa shughuli za misaada ya dharura wa Umoja wa Mataifa Jan Egeland ameelezea hali hiyo kuwa sawa na jinamizi huku majira ya baridi yakiwadia.
Egeland pia amesema helikopta zaidi zinahitajika kuwafikia wale walioko katika maeneo ya milima ya Himalaya.