Islamabad. Pakistan yashambuliwa tena na tetemeko.
24 Oktoba 2005Pakistan imeshambuliwa tena na tetemeko la ardhi, mara hii likiwa katika kiwango cha 6.0 katika kipimo cha Richter.
Hazikupatikana taarifa mara moja za maafa ama watu kujeruhiwa.
Tetemeko hilo la baada ya tetemeko kubwa lilitokea kiasi cha kilometa 140 kaskazini ya mji mkuu Islamabad katika jimbo la Himalaya katika eneo la Kashmir.
Karibu watu 80,000 wanafikiriwa kuwa wamekufa kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Oktoba 8 , wengi wao wakiwa ni kutoka kaskazini magharibi ya Pakistan .
Pakistan imekubali pendekezo kutoka India la kuweka kambi za misaada kwa ajili ya wahanga wa tetemeko hilo katika upande wake mpaka wa jimbo linalogombaniwa la Kashmir. Rais wa Pakistan Pervez Musharaff amewataka watu wa Kashmir kuruhusiwa kuvuka mpaka wa kusitisha mapigano ili kuweza kusaidiana kujenga upya maisha na nyumba zao.
Umoja wa mataifa umetoa wito kwa mataifa mbali mbali kutoa misaada zaidi, ukionya kuwa kunaweza kutokea wimbi jingine la vifo hadi pale misaada itakapowasili kwa ajili ya mamilioni ya watu ambao hawana makaazi kabla ya kuingia kwa majira ya baridi kali katika maeneo ya milima ya Himalaya.