ISLAMABAD: Pakistan yakumbwa na tetemeko lengine
13 Oktoba 2005Tetemeko lengine kubwa limetokea nchini Pakistan ambayo tayari inakabilana na kibarua kigumu cha kuwasaidia raia wake walionusurika tetemeko la Jumamosi iliyopita. Hakuna habari zilizotolewa kuhusu idadi ya majeruhi iliyosababishwa na tetemeko hilo la kipimo cha 5.6 kwenye kipimo cha Richter, lililotokea yapata kilomita 135 kazkazini mwa mji mkuu Islamabad. Takriban watu elfu 40 waliuwawa katika tetemeko la juma lililopita.
Habari zaidi zinasema miji iliyoathiriwa sana imeanza kupokea misaada kupitia helikopta za Marekani na Ujerumani, siku tano baada ya tetemeko la Jumamosi. Wanajeshi wa India wamevuka mpaka na kuingia Kashmir, kuwasaidia wanajeshi wenzao kujenga kambi zao zilizoharibiwa.
Serikali ya Pakistan inajaribu kuwapelekea chakula na mahema watu milioni mbili unusu walioachwa bila makao baada ya tetemeko la wiki iliyopita. Manusura wengi wanaoishi sehemu za milimani wamo hatarini kufariki dunia kwa sababu ya baridi kali.