IS wafanya shambulizi la kwanza dhidi ya serikali Syria
31 Mei 2025Hilo ni shambulizi la kwanza kufanywa na kundi hilo la kigaidi tangu kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.
Katika taarifa yake, IS imesema bomu moja lililoelekezwa kwenye gari la vikosi vya serikali lililipuka na kusababisha vifo vya wanajeshi 7.
Katika taarifa nyengine, kundi hilo limesema shambulizi jengine lilifanyika wiki hii likiwalenga wapiganaji wa kundi la Free Syrian Army wanaoungwa mkono na Marekani, IS imedai kuwa mpiganaji mmoja aliuwawa na wengine watatu walijeruhiwa katika shambulizi hilo.
Serikali ya Syria haijtoa tamko lolote kuhusiana na madai hayo ya Dola la Kiislamu.
Kundi la IS ambalo wakati mmoja lilikuwa linadhibiti sehemu kubwa za Syria na Irak, linaupinga utawala mpya wa Syria unaoongozwa na Rais Ahmad al-Sharaa, ambaye wakati mmoja alikuwa mkuu wa tawi la al-Qaeda nchini Syria ambapo alipambana na IS.