Iraq yaomba msaada wa dharura wa Dollar biliyoni nne
28 Februari 2004Matangazo
ABU DHABI: Mwanzoni mwa mkutano wa kimataifa wa ukarabati wa Iraq wa nchi fadhili, Baraza Tawala la Iraq limeiomba Jamii ya Kimataifa msaada wa dharura wa Dollar biliyoni nne za Kimarekani. Pesa hizo zimekusudiwa kugharimia miradi 700 muhimu, alisema Waziri wa Mpito wa Mambo ya Maendeleo Mehdi al Hafidh katika mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu. Wakati umewaadia kuwa Jamii ya Kimataifa itekeleze ahadi yake iliyotoa Oktoba mwaka jana mjini Madrid kwamba itaipa Iraq mkopo wa Dollar biliyoni 33 za Kimarekani, alidai Bwana Al Hafidh. Mkutano huo wa Abu Dhabi unaohudhuriwa na wawakilishi wa Marekani, UU, Japan, UM, Benki Kuu ya Dunia na Fuko la Kimataifa la Fedha unazungumzia mipango ya misaada na ugharimiaji ya kuikarabati Iraq.