Iran yatangaza nia ya kurejea kwenye mazungumzo ya nyuklia
24 Julai 2025Iran imesema leo kuwa iko tayari kuanza tena mazungumzo ya nyuklia na Marekani lakini kwa masharti kadhaa muhimu. Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa mambo ya Nje wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu Kazem Gharibabadi, siku moja kabla ya mkutano na mataifa yenye nguvu barani Ulaya utakaofanyika mjini Istanbul.
Mwanadiplomasia huyo wa Iran ameweka wazi kwamba mazungumzo ya nyuklia yanaweza kuanza tena alimradi haki za Tehran zilizoainishwa chini ya mkataba wa kuzuia uenezaji wa silaha za nyuklia NPT zitambuliwe.
Miongoni mwa masharti mengine ni Marekani kujenga uaminifu na Iran kwa kuonyesha nia njema na kuacha vitisho vya kijeshi pamoja na kutoa dhamana ya kutofanyika mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran wakati au baada ya mazungumzo hayo.
Masharti hayo yametolewa na Naibu Waziri wa mambo ya Nje wa Iran Kazem Gharibabadi, siku moja kabla ya mkutano huo wa Ijumaa mjini Istanbul utakayoyahusisha mataifa ya Ulaya - Uingereza, Ufaransa na Ujerumani almaarufu jumuiya ya E3.
Mazungumzo yatajikita kwenye kuondolewa vikwazo
Ingawa Marekani haijathibitisha ushiriki wake moja kwa moja, mazungumzo ya Istanbul yanatajwa kuwa huenda yakafungua njia ya kurejesha mazungumzo ya awali kati ya Tehran na Washington. Mazungumzo hayo yatakuwa ya kwanza tangu kuzuka kwa vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel mwezi uliopita na kufanyika kwa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran.
Mapema wiki hii, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei alisema kwamba mkutano huo utafanyika katika ngazi ya manaibu waziri wa mambo ya nje na pia utahudhuriwa na naibu mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya.
Baghaei amebainisha kwamba mazungumzo hayo yatajikita juu ya kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran na masuala yanayohusiana na mpango wa nyuklia wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ambapo itawasilisha matakwa yake bila uwoga na haitasita kutumia njia za kidiplomasia kulinda haki za raia wake.
Msemaji huyo wa wizara ya mambo ya nje ya Iran pia amezikosoa nchi tatu za Ulaya zilizotia saini makubaliano ya nyuklia ya mwaka 2015 kwa kile alichokiita kuwa na "msimamo usiofaa" na kusalia kimya kufuatia uchokozi wa Israel.
"Baada ya nchi nyingine kushindwa kutekeleza ahadi zao, Iran imepunguza matakwa yake hatua kwa hatua. Jumuiya ya E3 yenyewe pia imekosolewa kwa kutotimiza wajibu wao chini ya Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja (JCPOA). Kibaya zaidi, kufuatia uchokozi wa Israel, E3 hawakutoa tamko la kulaani bali walijaribu kuhalalisha mashambulizi ya Israel, kwa hivyo kama wanachama wa JCPOA, E3 hawana misingi ya kimaadili, kisiasa na kimantiki ya kutumia azimio ambalo wao wenyewe hawajalitekeleza la kurejesha vikwazo dhidi ya Iran."
Iran na jumuiya ya E3 zimefanya duru sita za mazungumzo tangu mwezi Septemba mwaka uliopita, wakati ujumbe wa pande zote ulipoanza majadiliano juu ya masuala kadhaa, ikiwa ni pamoja na mpango wa nyuklia wa Tehran na kuondolewa kwa vikwazo.
Duru ya mwisho ya mazungumzo hayo ilifanyika mjini Istanbul katikati ya mwezi Mei.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alisema mapema wiki hii kwamba vituo vya kurutisha madini ya Urani ya nchi hiyo vimeharibiwa vibaya kufuatia shambulio la Marekani. Alitia mkazo kwamba mpango wa kurutubisha madini hayo haujasimama na kwamba Iran haiwezi kuachana nao kabisa kwani unachukuliwa kuwa wa thamani kubwa na umefungamanishwa na heshima ya taifa.