Iran: Tumekuwa na mazungumzo ya wazi na mataifa ya Ulaya
25 Julai 2025Naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran Kazem Gharibabadi, aliyehudhuria mazungumzo hayo mjini Istanbul, Uturuki pamoja na mwanadiplomasia mkuu wa Iran Majid Takht-Ravanchi, wameandika katika mtandao wao wa X kwamba walitumia mkutano huo kukosoa msimamo wa Ulaya katika siku 12 za vita kati ya Israel na Iran.
Kazem Gharibabadi amesema pande zote zimekubaliana kwamba suala hilo litaendelea kujadiliwa katika mkutano ujao. Kabla ya mkutano huo duru kutoka Ulaya zilisema mataifa hayo matatu yanaitaka Iran kuweka wazi nia yake kuhusu urutubishaji wa madini yake ya urani na kufufua tena ushirikiano wake na wataalamu wa shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia IAEA.
Iran na mataifa ya E3 wakutana Istanbul kuhusu mpango wa Nyuklia
Hata hivyo Iran imesema iko tayari kujadili kuhusu viwango vya urutubishaji huo lakini sio haki ya kurutubisha madini yake. Jamhuri hiyo ya kiislamu pia imesisitiza kuwa haiwezi kamwe kuachana na mpango wake wa nyuklia.
Mataifa hayo matatu yanayojulikana kama E3 yalikuwa yametishia kuiwekea tena nchi hiyo vikwazo ilivyowekewa mwaka 2015, iwapo haitokubali kushiriki mazungumzo hayo na kukubaliana kuhusu viwango vya urutubishwaji wa madini yake ya Urani, na kutoa ushirikiano kwa wakaguzi wa IAEA.