Iran: Tutatoa pendekezo jipya la nyuklia kwa Marekani
9 Juni 2025"Hivi karibuni tutawasilisha pendekezo letu kwa upande mwingine ambao ni Marekani kupitia Oman, mara tu litakapokamilika. Ni pendekezo la busara, lenye mantiki na lisiloegemea upande wowote. Na tunapendekeza kwa dhati kwamba upande wa Marekani uthamini fursa hii. Hakika ni kwa manufaa ya wamarekani kuzingatia kwa uzito pendekezo hili," alisema Esmaeil Baqaei, Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Iran.
Spika wa bunge la Iran amesema pendekezo la Marekani lilikosa kujumuisha kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi, ambalo ni sharti muhimu kwa Iran kabla ya kufikiwa makubaliano yoyote na Marekani.
IAEA yasema Iran imeongeza urutubishaji madini ya urani
Mataifa hayo mawili yamekuwa na duru tano za mazungumzo tangu mwezi Aprili ili kuwa na makubaliano mapya ya nyuklia, kuchukua nafasi ya makubaliano yaliyofanyika awali na mataifa yaliyo na nguvu duniani, ambayo rais wa Marekani Donald Trump alijiondoa katika makubaliano hayo wakati wa awamu yake ya kwanza kama rais mwaka 2018.
Mahasimu hawa wawili wa muda mrefu wamekuwa katika mvutano mkubwa kuhusu urutubishwaji wa madini ya urani ya Iran huku jamhuri hiyo ya kiislamu ikisema ni haki yake kurutubisha madini hayo na Marekani nayo ikiielezea hali hiyo kucuka msitari mwekundu.