Iran yasema haitasita kujibu mashambulizi yeyote
26 Juni 2025Katika hotuba yake ya kwanza ya televisheni tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Iran na Israel, Khamenei amesema kuwa mashambulizi yoyote dhidi ya Jamhuri hiyo ya Kiislamu yatakuja kwa "gharama kubwa” akitaja kuwa Iran tayari ililenga kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani Mashariki ya kati, iliyoko Qatar, baada ya Marekani kujiunga na mashambulizi ya Israel.
Kama ilivyokuwa katika kauli zake zilizopita, zilizotolewa zaidi ya wiki moja iliyopita wakati wa siku 12 za mashambulizi ya Israel, alizungumza kutoka eneo lisilojulikana, mbele ya pazia zenye rangi kahawia, kati ya bendera ya Iran na picha ya mtangulizi wake Ayatollah Ruhollah Khomeini.
Aidha Khamenei amesema kwa kuzingatia uwezo wao wa kufikia maeneo muhimu ya Marekani katika Mashariki ya Kati na kuchukua hatua dhidi yao wakati wowote inapohisi sio jambo dogo.
"Katika moja ya matamshi yake, rais wa Marekani alisema kuwa Iran lazima ijisalimishe. Hili halihusiani tena na urutubishaji wa urani au sekta ya nyuklia pekee —ni juu ya kulazimisha Iran kunyenyekea. Bila shaka, kauli kama hiyo ni kujitutumua mno kutoka katika kinywa cha rais wa Marekani."
Rais wa Marekani Donald Trump alipoulizwa siku ya Jumatano iwapo Marekani ingeishambulia tena Iran alijibu "ndio" ikiwa Iran itatengeneza upya mpango wake wa kurutubisha madini ya urani.
Muswada wa kuachana na IAEA
Huku haya yakijiri mamlaka ya Iran yenye jukumu la kuidhinisha sheria imepitisha mswada wa kusitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, siku ya Alhamisi, ikieleza kuwa sababu ni mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani na Israel. Wabunge walipiga kura kuunga mkono muswada huo, siku moja baada ya usitishaji mapigano kumaliza vita vya siku 12dhidi ya Israel, ambapo Israel na Marekani zilishambulia maeneo ya nyuklia ya Iran.
Akizungumza na kituo cha televisheni cha serikali cha Iran IRNA, msemaji wa chombo hicho kinafahamika kama Baraza la Katiba, Tahan Nazif, amesema mswada huo, ambao sasa utawasilishwa kwa Rais Masoud Pezeshkian kwa idhini ya mwisho, utairuhusu Iran "kufaidika na haki zote zilizoainishwa chini ya Mkataba wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), hasa kuhusu urutubishaji wa urani.”
Tangu kuanza kwa vita tarehe 13 Juni, maafisa wa Iran wameikosoa vikali IAEA kwa kushindwa kulaani mashambulizi hayo. Aidha, Iran imekosoa azimio ililopitishwa na shirika hilo ambalo liliiishutumu Iran kwa kutotimiza majukumu yake ya nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amepinga hatua ya Iran iliyo mshirika mkuu wa Moscow, ya kusitisha ushirikiano na IAEA.