Iran yaonya kuhusu kurudishwa vikwazo vya UN
22 Julai 2025Iran imesema hatua ya kurudisha vikwazo vya kimataifa dhidi ya nchi hiyo itasababisha hali kuwa ngumu zaidi kuhusiana na mpango wake wa nyuklia.
Shirika la habari la taifa la Iran limemnukuu naibu Waziri wa Mambo ya Nje Kazem Gharibabadi ambaye ametowa mtazamo huo wakati akizungumza kuelekea mkutano uliopangwa kufanyika Ijumaa kati ya viongozi wa Iran na mataifa matatu ya Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.
Mataifa matatu ya kile kinachoitwa E3, yamesema ikiwa hakuna hatua itakayopigwa kufikia mwishoni mwa mwezi Agosti kuhusu mpango wa Nyuklia wa Iran, yataanzisha mchakato wa kuvirudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa, dhidi ya Tehran.
Vikwazo hivyo viliondolewa chini ya makubaliano ya mwaka 2015 baada ya Iran kukubali kupunguza urutubishaji madini ya urani.
Wakati huo huo, jana Jumatatu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alisema nchi hiyo inadhamiria kuendelea na mpango wake wa urutubishaji urani.