Iran yalaani vikwazo vipya ya Marekani
31 Julai 2025Siku ya Jumatano (Julai 30), Wizara ya Fedha ya Marekani ilitangaza vikwazo vipya dhidi ya watu, kampuni na meli 115 zinazohusishwa na kuwezesha uuzaji wa mafuta yaIrankwa Urusi.
Miongoni mwao ni meli zinazomilikiwa na Mohammad Hossein Shamkhani, mtoto wa kiume wa Ali Shamkhani, ambaye ni mshauri wa ngazi za juu wa masuala ya kisiasa kwa kiongozi wa juu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei.
Wizara ya Fedha ya Marekani ilidai kuwa Hossein Shamkhani anasimamia mtandao wa meli zaidi ya 50 za mafuta pamoja na meli zinazobeba makontena yanayosafirisha mafuta ya Iran na Urusi na bidhaa nyengine za petroli, na anazalisha faida ya mabilioni ya dola.
"Himaya ya usafirishaji ya familia ya Shamkhani inaonesha jinsi watawala wa Iran wanavyotumia nafasi zao kujikusanyia utajiri wa kutisha na kufadhili tabia za hatari za utawala huo." Alisema Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent.
Iran yalaani vikali
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran, Esmail Baqaei, alisema vikwazo hivyo ni "matendo yenye nia ovu yanayodhamiria kuyahujumu maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa watu wa Iran."
Baqaei aliongeza kuwa vikwazo hivyo ni ushahidi wa wazi wa uadui wa watawala wa Marekani dhidi ya Wairani na kuvielezea kuwa ni sawa na "uhalifu dhidi ya ubinaadamu."
Vikwazohivyo ndivyo vya kwanza vikubwa kabisa tangu utawala wa Trump uanzishe tena kile unachokiita "kampeni kubwa ya kuishinikiza Iran."
Tehran yadai fidia kwa vita vya Juni
Kwa upande mwengine, Iran ilitowa sharti kwa Marekani kuilipa fidia kwa madhara yaliyotokana na mashambulizi ya mwezi Juni dhidi ya Tehran yaliyoanzishwa na Israel na kisha Marekani kujiunga nayo kabla ya mazungumzo yoyote yale juu ya mpango wa nyuklia wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Akizungumza na jarida la Financial Times kwenye mahojiano yaliyochapishwa siku ya Alkhamis (Julai 31), Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Arraqshi, utawala wa Trump lazima utowe maelezo kwa nini uliishambulia katikati ya mazungumzo yaliyokuwa yakiendelea nchini Oman.
"Pia watowe hakikisho kwamba kamwe hawatarejea tena jambo kama hilo wakati tutakapozungumza tena. Na kisha lazima watufidie kwa hasara waliyotusababishia." Alisema Arraqshi.
Ripoti zinasema kwa muda wote wa vita hivyo vya siku 12 na hata baada ya hapo, Arraqshi na mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff, walikuwa wakiendelea kuwasiliana.
Arraqshi alimuambia Witkoff kwamba kulikuwa na haja ya kupata "suluhisho lenye manufaa kwa pande zote mbili" ili kuumaliza mkwamo wa muda mrefu kwenye mpango wa nyuklia wa Iran.
AFP, Reuters