Iran yakataa kusalimu amri
21 Februari 2005Tehran:
Serikali ya Iran leo imerudia usemi wake kuwa haitasalimu amri hata kidogo kwa mashinikizo yanayotolewa na Marekani na nchi za Ulaya za kuitaka iache mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium. Imetilia mkazo kwa kusema kuwa uwezo wake wa kinuklia hauwezi kuuzwa kamwe. Viongozi wa serikali ya Iran wamesema kuwa hawana nia ya kutengeneza silaha za kinuklia na wako tayari kutoa uthibitisho wa dhati kuwa mitambo yao ya kinuklia haitatumiwa kwa kutengenezea mabomu. Serikali ya Iran inashikilia kuwa ina haki ya kutekeleza mradi wa kurutubisha madini ya uranium kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Lakini Marekani inashuku kuwa kwa siri inajaribu kutengeneza bomu la atomiki. Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinajitahidi kuona kuwa suluhisho la amani linapatikana kuhusu mradi wa kinuklia wa Iran.