Iran yakataa kuingiliwa kuhusu nuklia.
10 Februari 2005TEHRAN:
Rais wa Iran Mohammed Khatami ameionya Marekani na mataifa ya Ulaya yanayoendeleza juhudi za kuizuia nchi yake kuwa na bomu la nuklia,kuwa kamwe Iran haitokuwa tayari kuweka hadharani mpango wake wa nuklia.
Rais huyo wa Iran pia ameonya madhara makubwa yanayoweza kutokea iwapo nchi yake haitotendewa haki kuhusiana na mpango wake wa nuklia,ambapo Iran mara kwa mara imekuwa ikieleza kuwa ni kwa ajili ya matumizi ya amani tu,huku Marekani ikiwa inaamini kuwa kuna siri inafichwa na watawala wa Iran kuwa wanatengeneza bomu la kinuklia.
Kiongozi huyo wa Iran amerudia uhakikishao wa nchi yake kuwa kamwe haitotengeneza silaha za nuklia kwa sababu wanapinga matumizi ya silaha hiyo.Hata hivyo akasema kuwa hawatakuwa tayari kuachana na mpango wa teknolojia ya nuklia kwa malengo ya amani.
Nako mjini Washington,rais George Bush wa Marekani ameitahadharisha dunia kuwa Iran ikiwa na silaha za kinuklia itakuwa ni nchi yenye nguvu kubwa za kijeshi duniani na akazitolea mwito nchi za magharibi kuzuia hilo lisitokee.