Iran yaiunga mkono Lebanon dhidi ya mashambulizi ya Israel
4 Juni 2025Waziri huyo amesema nchi yake inatazamiwa kuimarisha uhusiano wake na Lebanon hasa wakati huu baada ya kumalizika kwa vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hezbollah.
Ziara hiyo ya Abbas Araghchi inakuja baada ya mshirika wake mkuu nchini Lebanon, Hezbollah, kudhoofishwa vibaya na Isreal baada ya vita vyao vya kuwaunga mkono raia wa Palestina katika ukanda wa Gaza wanaokabiliwa na vita vya zaidi ya miezi 14.
Sehemu kubwa ya uwezo wa kijeshi wa kundi hilo la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran imepoteza nguvu huku ikishuhudia kuuawa kwa viongozi wake wakuu.
Ziara ya Araghchi ni ya kwanza tangu Oktoba mwaka uliopita siku chache kabla ya kumalizika kwa vita vya Israel na Hezbollah baada kusainiwa kwa makubaliano ya usitishaji mapigano uliosimamiwa na Marekani.
Vita hivyo viliua zaidi ya watu 4,000 nchini Lebanon, zaidi ya watu milioni 1 walilazimika kuyahama makazi yao na kusababisha uharibifu mkubwa nchini humo.
Mabilioni yanahitajika kuijenga upya Lebanon
Inaelezwa kwamba dola bilioni 11 zinahitajika ili kuweza kuyajenga upya maeneo ambayo yaliharibiwa na vita hivyo.
Ziara hiyo pia inakuja baada ya serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria kuondolewa madarakani mwezi Desemba. Assad alikuwa mmoja wa watu wa karibu wa Tehran na mshirika muhimu katika ulimwengu wa kiarabu na nchi yake ilikuwa kiungo muhimu kwa usafirishaji wa silaha kutoka Iran kuelekea Lebanon kwa kundi la wanamgambo la Hezbollah.
Wakati vita vilipokamilika, kamanda wa jeshi Joseph Aoun alichaguliwa kuwa rais wa nchi hiyo huku mwanasheria na mwanadiplomasia mashuhuri Nawaf Salam akichaguliwa kuwa waziri mkuu.
Katika mazungumzo yao, Aoun amemwambia afisa huyo wa Iran kwamaba Beirut iko tayari kuimarisha uhusiano wa nchi yake.
Iran: Tuko tayari kusaidia Lebanon
Itakumbukwa kwamba katika miongo kadhaa iliyopita, Iran iliifadhili Hezbollah kwa mabilioni ya dola na kupeleka kila aina ya silaha kwa kundi la hilo la nchini Lebanon.
Lakini tangu vita vya Israel na Hezbollah vilipoisha, mamlaka za Lebanon zimechukua hatua kali kwa kudhibiti nyanja zote za kundi hilo kupokea ufadhili huo kutoka kwa Iran.
Katika hatua nyingine Iran imelaani kukaliwa kwa mabavu kwa eneo la eneo la Lebanonna Isreal na imesema inaunga mkono jitihada zote zinachokuliwa na nchi hiyo kuwafukuza wavamizi ambao ni Israel.
Israel imekataa kuondoka katika maeneo matano ya Lebanon ambayo ilipaswa kuondoka tangu mwanzoni mwa mwaka huu baada ya kumalizika kwa vita.
Iran pia imeeleza nia yake ya kutaka kushiriki katika ujenzi mpya wa Lebanon ambayo imeharibiwa vibaya na vita lakini ikiwa nchi hiyo inataka hivyo.