Iran yafanya luteka ya kwanza tangu vita vyake na Israel
21 Agosti 2025Kwa mujibu wa televisheni ya taifa, meli za kijeshi za Iran zimerusha makombora kuelekea Ghuba ya Oman na Bahari ya Hindi.
Ingawa mazoezi hayo ya kijeshi ni ya kawaida katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu, mazoezi ya sasa yaliyopewa jina "Nguvu Endelevu 1404" yanafanyika wakati ambapo mamlaka nchini humo inajaribu kuonyesha uwezo wake wa kijeshi.
Iran inasisitiza kuwa iko tayari kukabiliana na kitisho chochote kutoka kwa Israel, hasa baada ya mifumo yake ya ulinzi wa anga na maeneo kadhaa ya nyuklia kuharibiwa katika vita hivyo viliyodumu siku 12.
Iran yasitisha uhusiano na IAEA
Wakati huo huo, Iran imesitisha ushirikiano wake na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA ambalo limekuwa likifuatilia shughuli za nyuklia nchini humo, huku Tehran ikichakata madini ya urani hadi kufikia viwango vinavyoweza kutumika kutengeneza silaha.
Israel iliishambulia Iran katika vita vya anga vilivyodumu kwa siku 12, ambavyo pia Marekani ilijiingiza kwa muda mfupi, na kushambulia vinu vikubwa vya nyuklia pamoja na kuwaua maafisa waandamizi wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia.
Iran yaahidi kujibu kwa nguvu shambulizi la maadui
Israel kwa kiasi kikubwa ilishambulia kambi za jeshi la anga wakati wa vita hivyo na inadhaniwa kwamba huenda kiasi kikubwa cha hifadhi ya makombora yake kiliharibiwa. Tangu wakati huo, Jamhuri ya Kiislamu ilisema iko tayari kwa mashambulizi yoyote dhidi yake katika siku za usoni.
"Mashambulizi yoyote mapya yatakayofanywa na adui yatajibiwa vikali," imesema sehemu ya taarifa yake iliyotolewa na Wizara ya Ulinzi siku ya Alhamisi. Rais wa Marekani, Donald Trump ametishia kuishambulia Iran kwa mara nyingine ikiwa itavifufua vinu vyake vya nyuklia, ikiwa ni pamoja na mitambo ya kurutubisha madini ya urani.
Tehran, imesitisha mazungumzo ya makubaliano na Washington yaliyolenga kudhibiti mipango ya taifa hilo ya nyuklia baada ya mashambulizi hayo ya Israel na Marekani, huku ikiendelea kukana madai kwamba inanuia kutengeneza bomu la nyuklia.