Iran yaanza kutekeleza adhabu kwa watuhumiwa wa ujasusi
25 Juni 2025Iran Jumatano (25.06.2025) imewanyonga watu watatu katika gereza la Urmia, mkoani West Azerbaijan, kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa niaba ya Israel na kuingiza nchini vifaa vya mauaji. Wafungwa hao waliotambulika kama Azad Shojaei, Edris Aali, na Rasoul Ahmad Rasoul – raia wa Iraq – walikuwa kwenye orodha ya wale waliowahi kutajwa na shirika la Amnesty International kuwa wako hatarini kunyongwa bila haki ya rufaa.
Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, IRNA, hii inafanya idadi ya watu walionyongwa kwa tuhuma za ujasusi kuwa sita tangu Juni 16 – hali ambayo imezua wasiwasi miongoni mwa wanaharakati kuwa wimbi la adhabu linaweza kuendelea hata baada ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha vita na Israel.
Wakati huo huo, Bunge la Iran limepitisha hatua ya kusitisha ushirikiano na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki, IAEA, likilituhumu kwa kushindwa kulaani mashambulizi ya Marekani na Israel dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Ghalibaf, amesema kuwa ushirikiano wowote hautarejeshwa hadi usalama wa vituo hivyo utakapohakikishwa.
Trump atetea mashambulizi ya jeshi la Marekani nchini Iran
Lakini kwa upande wa Marekani, Akiwa nchini Ulolanzi kwenye mkutano wa kilele wa Jumuiya ya NATO, Rais Donald Trump amesema kwamba taarifa za kijasusi kufuatia mashambulizi kwenye maeneo ya nyuklia ya Iran hazikuwa na uhakika. Amesema mashambulizi hayo yameleta madhara makubwa zaidi kuliko inavyoripotiwa kwenye mitandao ya habari.
Katika mkutano wa hadhara huko Ohio, Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, alizungumza kuhusu kile alichokiita "Dhana ya Trump” – akitolea mfano Iran kama ushahidi wa mafanikio ya mbinu hiyo.
"Ninachokiita Dhana ya Trump ni rahisi sana. Kwanza, unaweka wazi maslahi ya Marekani — na katika kesi hii, ni kwamba Iran haiwezi kuwa na silaha za nyuklia. Pili, unajaribu kwa nguvu na kidiplomasia kutatua tatizo hilo. Na tatu, ikiwa haliwezi kutatuliwa kwa njia ya kidiplomasia, unatumia nguvu kubwa za kijeshi kulitatua, kisha unajiondoa haraka kabla hali haijageuka kuwa vita ya muda mrefu. Hiyo ndiyo Dhana ya Trump", alisema Vance.
IAEA yataka kufikia maeneo ya nyuklia
Mkuu wa shirika la nyuklia la Umoja wa Mataifa, Rafael Grossi, amesema kipaumbele cha juu kwa wakaguzi wake ni kurejea katika vituo vya nyuklia vya Iran ili kutathmini athari za mashambulizi ya kijeshi ya hivi karibuni. Grossi amesisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Tehran unahitaji suluhisho ya kidiplomasia.
Wakati hali ya usalama ikionekana kutulia, serikali ya Iran imepanga kufanya mazishi ya kitaifa Jumamosi hii kwa makamanda na wanasayansi waliouawa katika mashambulizi ya Israel, akiwemo Hossein Salami– mkuu wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi aliyeuawa siku ya kwanza ya vita.
Soko la mafuta na mitaji duniani limeanza kuonesha matumaini, huku wawekezaji wakipata ahueni baada ya kusitishwa kwa vita. Bei ya mafuta imeshuka kwa zaidi ya asilimia 16 tangu kilele cha mzozo, ingawa bado kuna wasiwasi iwapo usitishaji huu wa vita utadumu.
Katika tukio jingine la kushangaza, Rais Trump alisema China inaweza kuendelea kununua mafuta kutoka Iran licha ya vikwazo vya Marekani, kauli ambayo wachambuzi wameitafsiri kama njia ya kuweka shinikizo mpya kwenye mazungumzo ya nyuklia yajayo.