Iran yaahirisha uamuzi kuhusu mradi wake wa kinuklia
4 Agosti 2005Serikali ya Iran imetangaza hapo kabla kuwa ingalianza shughuli zake za kubadilisha madini ya uranium kuwa gesi jana Jumatano. Lakini baadaye ikatangaza kuwa zimeahirishwa mpaka Jumamosi ijayo ili kuwa na muda mrefu wa mazungumzo ya kidiplomasia.
Kaimu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Tom Casey, amewaambia Wandishi wa Habari, “Ni jambo zuri kuona kuwa Wairan wamebatilisha uamuzi wao.”
Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya amesema mjini Brussels kuwa muda mpya uliowekwa na Wairan ni hatua inayofaa.
Amesema, “Hii ni ishara kuwa uhusiano bado haujavunjwa na ya kwamba Iran inataka kufahamu zaidi kuhusu mapendekezo yatakayotolewa na nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.”
Mkuu wa sera za nchi za nje wa Umoja wa Ulaya, Javier Solana, amesema kuwa Rais mpya wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, aliyeanza wadhifa wake leo anakabiliwa na uchaguzi wa kimbinu. Aendelee kufuata njia itakayomtenga au anufaike na marupurupu ya ushirikiano wa kimataifa.
Marekani na nchi za Ulaya zimesema dhahiri shahiri kuwa hatua zozote zile za kurudia harakati za kurutubisha madini ya uranium, zilizosimamishwa kutokana na mapatano yaliyofikiwa mwezi wa Novemba mwaka wa jana, zitazisababisha ziunge mkono Iran kuwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa.
Uamuzi wa Iran sasa utazipa muda zaidi Uingereza, Ufaransa na Ujerumani kutayarisha mapendekezo ya kuisaidia nchi hiyo kiuchumi na kiulinzi ili iweze kuacha mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje amesema kuwa Umoja wa Ulaya umeiarifu Marekani kuwa utafichua mpango wake wa kuisaidia Iran kabla ya mwisho wa juma hili.
Nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinaripotiwa kuwa ziko tayari kuwathibitishia Wairan kuwa watapata mafuta ya kutosha kwa ajili ya kiwanda chao cha kinuklia kinachojengwa Bushehr pamoja na viwanda vingine vitakavyojengwa baadaye mahali pengine.
Msaada huo pia utahusu marupurupu ya kibiashara, ndege za kiraia na vipuri vyake vinavyohitajiwa sana, kuisaidia nchi hiyo ijiunge na Shirika la Biashara Ulimwenguni (WTO) na kuirudisha tena katika mazungumzo ya ulinzi ya kimkoa.
Wairan wanashikilia kuwa mradi wao wa kinuklia ni kwa ajili ya matumizi ya kiraia. Lakini Wamarekani wanaamini kuwa hiyo ni mbinu ya kutaka kurutubisha madini ya uranium ili baadaye waweze kutengeneza bomu la kinuklia.
Kiongozi Mkuu wa kidini wa Iran, Ali Khamenei, amesema kuwa maadui wa Iran, wakiongozwa na shetani mkubwa Marekani, wanafahamu bayana kuwa Iran haitasalimu amri.
Akaongeza kusema, “Viongozi wa Iran hawana haki hata kidogo ya kuacha masilahi ya kiuchumi na kisiasa ya taifa. Haki hizi lazima zilindwe.”
Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni (IAEA) limekuwa likichunguza mradi wa kinuklia wa Iran tokea mwezi wa Februari mwaka wa juzi kutokana na tuhuma za Marekani kuwa Jamhuri ya Kiislamu imo mbioni kutengeneza silaha za kinuklia.
Marekani inataka suala la Iran lijadiliwe kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Ingawaje inaunga mkono juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu dhidi ya nchi hiyo.