Iran yaanza mazungumzo na mataifa ya E3, Istanbul
25 Julai 2025Mazungumzo kuhusu mpango wa Nyuklia kati ya Iran na wajumbe kutoka Uingereza,Ufaransa na Ujerumani, yameanza hivi leo nchini Uturuki.
Katika mazungumzo hayo Iran itahitajika kutoa ahadi kuhusu masuala kadhaa ikiwemo kuridhia kuingia kwenye mazungumzo na Marekani.
Mazungumzo kati ya Iran na kile kinachojulikana kama E3 yaani mataifa matatu ya Ulaya, Uingereza,Ufaransa na Ujerumani yanaendelea katika ubalozi mdogo wa Iran mjini Istanbul na yanatarajiwa kumalizika mchana huu.Soma pia:EU yatishia kuirejeshea Iran vikwazo isipofikia makubaliano ya nyuklia
Na kwenye mkutano huo wa moja kwa moja na mataifa yenye nguvu ya magharibi, inaelezwa kwamba Iran imeshayakataa mapendekezo ya kuendelea na azimio la Umoja wa Mataifa lililoidhinisha makubaliano ya Nyuklia ya mwaka 2015.
Mazungumzo ya hivi leo ni ya kwanza kufanyika kati ya mataifa ya magharibi na Iran tangu nchi hiyo iliposhambuliwa na Israel na Marekani mwezi uliopita na maeneo yake ya Nyuklia kuharibiwa. Lakini pia yanafanyika huku yakiweko maswali kuhusu hatma ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Nchi za Ulaya pamoja na China na Urusi ndio pekee waliobaki katika makubaliano ya nyuklia ya 2015 baada ya Marekani kujitowa mwaka 2018.
Itakumbukwa kwamba Iran iliondolewa vikwazo vya Umoja wa Mataifa chini ya makubaliano hayo kwa nchi hiyo kutakiwa kukubali kuwa chini ya uangalizi wa IAEA. Lakini azimio linalosimamia mkataba huo wa Nyuklia muda wake unafikia mwisho Oktoba 18 na Iran inasema haitokubali kurefushwa kwa muda wa azimio hilo.
Muda mfupi kabla ya kuanza mazungumzo ya Istanbul msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Iran Esmaeil Baghaei alisema Tehran inautazama mjadala kuhusu kufikiria kurefusha muda wa azimio nambari 2231 la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kama usiokuwa na maana na wala hauna msingi.Soma pia:Nchi tatu za Ulaya zatishia kurejesha vikwazo kwa Iran
Iran itatakiwa kutoa ahadi kuhusu masuala kadhaa ikiwemo kuzungumza na Washington, kutoa ushirikiano kamili na shirika la atomiki duniani IAEA pamoja na kuwa wazi kuhusu kilogramu 400 ya madini ya Urani yaliyorutubishwa ambayo hayajulikani yaliko.
Na kwahivyo kundi la E3 linataka kuishawishi Iran iingie kwenye mazungumzo na imeweka muda wa hadi mwishoni mwa mwezi Agosti wa kuanzishwa juhudi za kidiplomasia, vinginevyo zitaanzisha mchkato wa kurudisha vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo wanadiplomasia wa Ulaya na Iran wanasema hakuna matumaini ya Iran kurudi tena kwenye meza ya mazungumzo na Marekani kwa hivi sasa.
Rais Masoud Pezeshkian kwenye mahojiano na kituo cha Aljazeera yaliyorushwa Jumatano,kiongozi huyo wa Iran alisema Tehran imeajiandaa kwa vita nyingine huku akisisitiza kwamba mpango wa Nyuklia wa nchi hiyo utaendelea chini ya sheria ya kimataifa na Iran haina dhamira ya kutengeneza silaha za Nyuklia.