Iran na Marekani zarejea tena mezani mazungumzo ya nyuklia
23 Mei 2025Wajumbe wa pande hizo mbili waliwasili kwenye jengo la ubalozi wa Oman mjini Roma mnamo adhuhuri leo Ijumaaa kuanza duru nyingine ya mazungumzo kuhusu mradi wa nyuklia wa Iran.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi na mjumbe maalumu wa Rais Donald Trump kwenye kanda ya mashariki ya kati Steve Witkoff ndio wanatazamiwa kuongoza mazungumza hayo chini ya upatanishi wa Oman.
Tehran imetahadharisha kuwa kupatikana makubaliano itakuwa suala gumu kutokana na masharti yasiyoyumba yaliyowekwa na kila upande.
Majadiliano yasasa yatajikita kwenye suala la urutubishaji madini ya urani unaofanywa na Iran. Hili ni suala gumu zaidi hasa ikizingatiwa kila upande hauoneshi ishara ya kubalidi msimamo wake.
Marekani inataka Iran iachane kabisa na urutubishaji madini ya urani, kwa mashaka kuwa Tehran inaweza kuyatumia kuunda bomu la nyuklia.
Takwa hilo linapingwa vikali na viongozi wa Iran na waziri Araghchi amesema kabla ya kuanza mazungumzo kuwa kamwe Tehran haitokubali kulazimishwa kuacha kurutubisha urani.
Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa X, mwanadiplomasia huyo amesema iwapo Marekani itailazimisha Iran isitishe kabisa urutubishaji madini hayo, basi "hakutakuwa na mkataba wowote" kati ya pande hizo mbili.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmael Baghaei amesema Iran haitosita kuikabili Washington kwenye meza ya mazungumzo.
"Kutokana na misimamo isiyoeleweka na yenye kubadilika kila wakati ambayo tunaisikia kutoka kwa maafisa wa Marekani kwa wiki hii nzima, pamoja na awamu nyingine ya vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni wazi kuwa tutayazusha masuala hayo haraka sana mezani na kwa uzito mkubwa tutakapokutana na upande wa pili kwenye mazungumzo haya"
Rubio asema haitokuwa rahisi kufikia makubaliano na Iran
Marekani yenyewe kupitia msemaji wake wa Ikulu ya White House, Karoline Leavitt imesema Rais Trump anaamini mazungumzo na Iran "yanakwenda katika mwelekeo sahihi".
Hata hivyo licha ya ugumu unaoyagubika mazungumzo hayo, kila upande unaonesha kutambua umuhimu wake.
Rais Trump anataka kwa kila hali kupunguza uwezekano wa Iran kuunda silaha za nyuklia kwa wasiwasi kwamba hatua inaweza kuchochea mashindano ya kuunda silaha hizo za maangamizi kwenye kanda ya Ghuba na Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake Tehran inahitaji kuondolewa mbinyo kupitia vikwazo vikali vya kiuchumi vilivyowekwa na Washington vinavyouathiri pakubwa uchumi wake unaotegemea zaidi nishati ya mafuta.
Kisiki kikubwa itakuwa ni kwa Washington kuishawishi dola hiyo ya Uajemi kuupa kisogo mradi wake wa nyuklia.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Marco Rubio amesema Washington inataka kupata mkataba utakaoiruhusu Iran kuwa mradi wa nyuklia wa kiraia lakini usiojumuisha urutubishaji madini ya urani.
Hata hivyo amekiri kufikia makubaliano ya aina hiyo "haitokuwa kazi rahisi". Marekani na mshirika wake wa karibu kwenye kanda ya mashariki ya kati Israel, wanashuku kuwa Iran huenda tayari imefikia uwezo wa au inakaribia kuunda bomu la nyuklia kupitia madini iliyorutubisha.
Tehran lakini inasema haina mpango huo na mradi wake ni salama na ni kwa matumizi ya kiraia.