Iran: Mtetemeko wa ardhi wauwa watu 20,000.
27 Desemba 2003Matangazo
TEHERAN: Watu wapatao 20,000 wameuawa katika balaa kubwa la mtetemeko wa ardhi huko Iran, Kusini-Mashariki, iliarifu Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi. Watu zaidi ya 30,000 wamajeruhiwa, ilisema taarifa ya Wizara hiyo iliyosomwa katika Televisheni ya Taifa. Ripoti nyingine zinataja hadi majuruhi 50,000. Katika mji wa BAM ulioteketezwa karibu wote, watu wapatao 10,000 walilala nje katika baridi kali kwa sababu ya kuteketezwa nyumba zao. Makundi ya kuokoa watu yakisaidiwa na mbwa, yanaendeleza juhudi zao za kuwatafuta watu wengine ambao huenda wamenusurika. Upande mwengine, hata masaa 24 baada ya kutokea balaa hilo, maelfu ya watu wanabidi kujitegemea wenyewe katika vijiji vilivyokatiwa mawasiliano. Ripoti za Televisheni ya Iran zimesema makundi ya kuokoa watu yameshindwa kuwasili sehemu hizo za mbali.