Iran kurudia mradi wake wa kinuklia
10 Mei 2005Tehran:
Iran itaamua katika siku chache zijazo kama irudie mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium au la! Mradi huo umesimamishwa ikiwa ni sehemu ya mapatano na Umoja wa Ulaya. Msemaji wa Baraza Kuu la Taifa la Ulinzi la Jamhuri ya Kiislamu, Ali Agha Mohammadi, amesema kuwa Maafisa, pamoja na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Kamal Kharazi na Wabunge wenye msimamo mkakamavu, watakutana na kuchukua uamuzi katika mazungumzo yao ya leo na kesho Jumatano. Wanadiplomasia wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani wamesema kuwa Iran kurudia mradi wake kutachukuliwa kuwa imevunja mkataba wa kusimamisha harakati hizo wa mwezi wa Novemba mwaka wa jana. Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, kutokana na mapatano hayo, zimekuwa tayari kuanzisha mazungumzo na Iran. Ikiwa Iran itaendelea na mradi wake, nchi hizi zitashirikiana na Marekani katika kuiwasilisha Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambako huenda ikawekewa vikwazo.