Iran kufikishwa mbele ya Baraza la Usalama
20 Septemba 2005Matangazo
Vienna:
Wajumbe wa Umoja wa Nchi za Ulaya wametayarisha azimio na kulikabidhi Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki kuhusu mgogoro wa nishati hiyo na Iran. Azimio hilo litawasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa iwapo muwafaka hautafikiwa. Azimio linaliarifu Baraza la Usalama kuwa Iran imeshindwa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia silaha za kinuklia. Baraza la Usalama linaweza kuiwekea Iran vikwazo. Nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Ujerumani, Ufaransa na Uingereza, kwa niaba ya Umoja huo, zimejitahidi bila ya mafanikio kuona kuwa Iran inaacha mradi wake wa kurutubisha madini ya uranium ambayo yanaweza kutengeneza bomu la kinuklia na badala yake ipewe misaada ya kiuchumi.