Iran kuchukuliwa hatua kali?
9 Agosti 2005Makamu wa Rais wa Shirika la Nishati ya kinuklia wa Iran, Mohammad Saidi, ametangaza jana kuwa nchi yake imerudia harakati zake za kubadilisha madini ya uranium kuwa gesi katika kiwanda cha Isfahan.
Shughuli hizo ziliahirishwa miezi tisa iliyopita kutokana na mapatano yaliyofikiwa wakati ule kati ya Iran na nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani na Marekani.
Umoja wa Ulaya, kutokana na uamuzi huo wa Iran, umeitisha leo kikao cha dharura cha Kamati Kuu ya Shirika la Nishati ya Atomiki Ulimwenguni (IAEA). Mkutano unatazamiwa kuipa Iran muda wa mwisho wa kusimamisha harakati zake za kubadilisha madini ya uranium kuwa gesi.
Mkutano wa leo mjini Vienna, Austria ni hatua ya kwanza ya mwenendo ambao huenda suala hilo likajadiliwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na baadaye Iran kuwekewa vikwazo.
Hivyo ndivyo Marekani ilivyokuwa inataka kinyume na nchi za Umoja wa Ulaya ambazo zimetaka kuepusha jambo kama hilo.
Marekani ingawaje inaunga mkono juhudi za kidiplomasia za Umoja wa Ulaya lakini haijaondoa uwezekano wa kutumia nguvu dhidi ya nchi hiyo.
Shirika la IAEA katika mkutano wake muhimu wa leo lingalipendelea kuionya vikali Iran badala ya kuifikisha moja kwa moja katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Maafisa wa Iran hata hivyo wametilia mkazo kwa kusema kuwa hawana wasiwasi hata kidogo kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wanadai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ina haki ya kutengeneza mafuta ya kinuklia kwa mujibu wa mkataba wa kuzuia utengenezaji wa silaha za kinuklia (NPT).
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, amemwomba Rais mpya wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad, kutumia busara zaidi kuhusu msimamo wa nchi yake kuelekea nchi za magharibi katika mradi wake wa kinuklia.
Msemaji wa Annan, Stephane Dujarric, amesema kuwa katika mazungumzo yake na Rais wa Iran, Kofi Annan amemsihi aendelee na mwenendo wa sasa hivi.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatumaini kuwa pande zinazohusika zitajitahidi kutafuta suluhisho linalokubalika.
Nchi tatu za Umoja wa Ulaya, Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimesema kuwa Iran kurudia harakati zake za kinuklia hapo jana kumezusha mgogoro mkubwa wa kimataifa unaohitaji jibu moja la jamii ya kimataifa.
Waziri wa Mambo ya Nchi za nje wa Ujerumani, Joschka Fischer, ameonya uwezekano wa Iran kuchukuliwa hatua kali ambazo zitaiathiri nchi hiyo.
Marekani imesema kuwa uamuzi wa Iran unavunja mapatano yaliyofikiwa mjini Paris, Ufaransa na nchi za Umoja wa Ulaya. Kwa hiyo, itatangaza msimamo wake baada ya kushauriana na Uingereza, Ufaransa na Ujerumani.
Naibu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Adam Ereli, amesema kuwa mradi wa kinuklia wa Iran umejaa uongo na siri kubwa. Kila kitu kitafanywa kuhakikisha kuwa nchi hiyo haitengenezi silaha za kinuklia.