Iran: Hatuna chaguo ila kutumia silaha za nyuklia kwa US
3 Aprili 2025Ali Larijani, Mshauri wa kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, amesema kwenye mahojiano na televisheni ya taifa la Iran kwamba "hawaelekei kwenye kuunda silaha za nyuklia, lakini ikiwa Marekani itafanya makosa katika swala hilo basi Iran italazimika kuelekea kwenye mkondo huo kwa sababu inapaswa kujilinda."
Kauli hii ameitoa saa chache baada ya kiongozi mkuu Ayatollah Ali Khamenei, kuahidi kuijibu Marekani endapo Trump atatimiza tishio lake la kulishambulia taifa hilo la Kiislamu.
Soma pia:Iran yasema italipiza kisasi ikiwa itashambuliwa na Marekani
Larijani amesisitiza kauli hiyo ya Kiongozi Mkuu kwamba Iran italazimika kuchukua hatua tofauti iwapo Marekani itaishambulia nchi yake kwa mabomu au kupitia kwa Israel.
"Tumesema kuna amri ya kidini inayokataza kutengeneza silaha za nyuklia, tunatoa ushirikiano kwa shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia (IAEA) na hivyo hatupangi kujielekeza kwenye silaha ya nyuklia, lakini Marekani ikifanya makosa kuhusiana na suala la nyuklia la Iran, itatulazimisha kufuata njia hiyo, kwa sababu Iran inapaswa kujilinda."
Katika mahojiano siku ya Jumamosi, Trump alisema "yatafanyika mashambulizi ya mabomu" ikiwa Iran haitakubali kufikia makubaliano mapya ya nyuklia. Kulingana na shirika la habari la NBC, Trump pia alitishia kuiadhibu Iran kwa kuiwekea vikwazo vya ushuru".
Iran: Tishio la Trump ni dharau kwa mataifa
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baqaei, amesema kupitia chapisho kwenye mtandao wa X, kwamba tishio hilo linaashiria "kudharau amani na usalama wa kimataifa, ambalo ni jambo la kushangaza".
Ameonya juu ya "matokeo" ambayo hayajabainishwa iwapo Merekani itachagua njia ya "vurugu".
Wizara ya mambo ya nje ya Iran pia iliitisha kikao na ubalozi wa Uswizi, ambao unawakilisha maslahi ya Marekani nchini Iran hapo jana Jumatatu, kupinga vitisho vya rais Donaldtrump. Marekani ina kambi 10 katika eneo karibu na Iran, na jumla ya wanajeshi 50,000.
Soma pia:Iran yakataa mazungumzo na Marekani
Tangu aingie madarakani mwezi Januari, Trump amerejesha sera yake ya kushinikiza, ambayo katika muhula wake wa kwanza aliiondoa Marekani kutoka kwenye makubaliano ya kihistoria kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na akaiwekea tena vikwaz nchi hiyo.