Iran: Duru ya pili mazungumzo na Marekani itafanyika Roma
17 Aprili 2025Tangazo kuhusu kufanyika kwa mazungumzo yajayo mjini Roma, Italia limetolewa na televisheni ya taifa ya Iran jana jioni.
Taarifa imearifu kwamba Oman iliyokuwa mwenyeji wa mkutano wa mwanzo itaendelea kuwa msuluhishi katika mazungumzo hayo ya awamu ya pili siku ya Jumamosi.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Oman, ndiye alikuwa kiungo wa mashauriano ya awali kati ya Washington na Tehran mjini Muscat wikendi iliyopita.
Hadi Jumanne wiki hii Iran ilikuwa imesisitiza itarejea tena Oman kwa mazungumzo ya duru ya pili licha ya maafisa wanaosimamia mazungumzo hayo kutangaza siku ya Jumatatu kuwa Roma ndiyo itakuwa eneo la mazungumzo yanayofuata.
Hata hivyo maafisa wa Marekani hawajasema hadharani hadi sasa mahali mazungumzo yajayo yatakapofanyika lakini Rais Donald Trump alizungumza kwa njia ya simu na Mfalme Haitham bin Tariq wa Oman siku ya Jumanne.
Iran yakataa sharti la kuachana na urutubishaji madini ya Urani
Haijafahamika hadi sasa ajenda kuu za mkutano wa Jumamosi zitakuwa zipi lakini Iran tayari imeondoa uwezekano wa kujadili suala la kuachana na urutubishaji madini ya Urani.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran Abbas Araghchi, amesema haki ya Iran kurutubisha madini hayo haiwezi kuwa sehemu ya majadiliano.
Alikuwa akijibu matamshi ya mwakilishi mkuu wa Marekani kwenye mazungumzo kati ya pande hizo mbili Steve Witkoff aliyesema watawala mjini Tehran ni sharti "wasitishe na kuachana kabisa na urutubishajii madini ya Urani" ili kufikia mkataba na Washington.
"Mkutano wa Jumamosi utakuwa ni mwendelezo wa ule uliopita. Kama tulivyoeleza, mazungumzo yaliyopita yalikuwa ya kujenga na yenye matarajio fulani. Hata hivyo, kati ya awamu ile ya kwanza na hii ya sasa, tumesikia misimamo kadhaa na wakati mwingine yenye utata kutoka maafisa wa Marekani, ambayo kwa maoni yangu hayatosaidia kuleta mwelekeo mzuri wa majadiliano haya". amesema Waziri Araghchi.
Pande hizo mbili zinajaribu kutafuta mkataba utakaopunguza uhasama uliochochewa na mradi wa nyuklia wa Iran ambao Marekani inashuku unaweza kutumiwa na nchi hiyo kuunda silaha za nyuklia.
Hivi karibuni Rais Donald Trump wa Marekani alitishia kuishambulia Iran ikiwa itaweka vizingiti vya kupatikana mkataba wa kuukongoa mradi wake wa nyuklia. Tehran ilijibu kwa kumwonya Trump kwamba vitisho na ubabe haviwezi kuitikisa dola hiyo ya uajemi.
Mkuu wa IAEA ziarani Tehran kwa mazungumzo na maafisa wa Iran
Wakati mkutano wa Jumamosi unasubiriwa, Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nguvu za Atomiki, IAEA, Rafael Grossi yuko nchini Iran tangu jana kwa mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo.
Amepangiwa kuwa na mkutano na Rais Masoud Pezeshkian na maafisa wengine. Alipowasili alikutana na Waziri Araghchi, ambapo inaarifiwa alifahamishwa juu ya kile kilichojadiliwa kwenye mazungumzo ya awali yaliyofanyika Muscat, Oman.
Araghchi, pia amemtolea Grossi kuhakikisha shirika analoliongoza linachukua msimamo wa wazi kuhusiana na vitisho vinavyotolewa dhidi ya miundombinu ya nyuklia ya Iran.
Marekani na Israel zote zimeapa kuilenga miundombinu hiyo iwapo hakuna mkataba utakaopatikana na Iran.
Grossi anatarajiwa vile vile kujadili suala la ya ruhusa ambayo wakaguzi wa IAEA watapatiwa katika kusimamia utekelezaji wa makubaliano yoyote yatakayofikiwa kati ya Iran na Marekani.