Makoloni ya zamani ya Ufaransa, miaka 65 baada ya Uhuru
26 Agosti 2025Licha ya mafanikio fulani, changamoto kubwa bado zinayakabili mataifa mengi ya Afrika yanayotumia lugha ya Kifaransa- Francophonie. Takwimu za Faharasi ya Maendeleo ya Binadamu (HDI) zinaonyesha nchi nane kati ya 14, ikiwemo zile za Ukanda wa Sahel kama Mali, Burkina Faso, Niger na Chad, bado zipo kwenye kiwango cha chini kabisa cha maendeleo. Wachambuzi wanasema mchanganyiko wa uwezo duni wa sekta ya kilimo, ongezeko kubwa la watu, na ukosefu wa utulivu wa kisiasa umezuia maendeleo.
Katika miaka ya karibuni, mapinduzi ya kijeshi yameondoa serikali za kidemokrasia katika nchi kama Mali, Burkina Faso na Niger, huku katika mataifa mengine viongozi wa muda mrefu wakishikilia madaraka kwa miongo mingi. Mfano ni Paul Biya wa Cameroon, mwenye umri wa miaka 92, anayepanga kugombea tena, na Faure Gnassingbé wa Togo, aliyebadilisha katiba ili kuendelea kutawala bila ukomo.
Wataalamu wanasema kuwa ndoto za miaka ya 1990 za kujenga taasisi imara zimeyeyuka, zikibadilishwa na siasa zinazoendeshwa na "watawala wa kimabavu” wanaopuuza katiba na demokrasia. Hali hii imetajwa kama moja ya sababu zinazodidimiza maendeleo na kuendeleza migogoro.
Ufaransa, ambayo bado ina uhusiano wa kihistoria na mataifa haya, sasa inaona ushawishi wake wa kisiasa ukipungua. Baada ya mapinduzi katika nchi za Sahel, vikosi vya kijeshi vya Ufaransa vimeondolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Urusi. Hata hivyo, misingi ya kisiasa na kikatiba ya nchi nyingi bado inabeba alama za Kifaransa, kama anavyoeleza Matthias Basedau, Mkurungezi wa taasisi ya utafiti wa Afrika ya GIGA, yenye makao yake mjini Hamburg, Ujerumani.
"Kuna huu mfumo wa urais, ambao hata hivyo una mamlaka makubwa zaidi na wa kiimla zaidi kuliko ule wa Ufaransa usiyo na mamlaka makubwa. Na katiba nyingi zimeundwa kwa kufuata mfano wa Kifaransa. Kipengele cha kipekee hapa kinachohusu kutofautisha kabisaa dini na dola. Mtu anaweza hata kusema kuwa hii imechangia kupunguza ubaguzi wa kidini katika eneo hilo."
Hata hivyo, ushirikiano wa kiuchumi bado ni mkubwa. Sekta za mafuta, madini, biashara, na huduma za mawasiliano zinaendelea kudhibitiwa na kampuni za Kifaransa. Pia, mataifa mengi ya Afrika Magharibi na Kati bado yanatumia sarafu za Faranga -CFA, ambazo mara nyingi hukosolewa kwa kudumisha utegemezi wa kifedha, ingawa zinasaidia kudhibiti mfumuko wa bei na kurahisisha biashara.
Mabadiliko pia yanaonekana katika mchango wa diaspora. Nchini Senegal, kwa mfano, takriban Wasenegali 110,000 wanaoishi Ufaransa huchangia zaidi ya asilimia 10 ya pato la taifa kupitia fedha wanazotuma nyumbani, zikisaidia moja kwa moja familia nyingi vijijini.
Licha ya changamoto za kisiasa na kiuchumi, kuna hatua za maendeleo. Idadi ya watu wanaoishi katika umaskini wa kupindukia imepungua, maisha ya binadamu yameongezeka, na vifo vya watoto wachanga vimepungua ikilinganishwa na miaka ya awali ya uhuru.
Miaka 65 baada ya "Mwaka wa Afrika,” mataifa ya Francophonie barani Afrika yamepiga hatua mseto: baadhi yakijaribu kujinasua kutoka kivuli cha ukoloni huku mengine yakibaki na utegemezi wa kifedha na kiusalama kwa mataifa ya kigeni.