Ipi hali ya uchumi duniani kufuatia mzozo wa Iran na Israel?
13 Juni 2025Bei ya mafuta imepanda kwa kasi, wawekezaji wamekimbilia maeneo salama ya uwekezaji, huku uchumi wa dunia ukihofiwa kuwa utadorora.
Mashambulizi ya leo alfajiri yaliyofanywa na Israel katika vituo vya Iran vya nyuklia na makombora, yamesababisha mtikisiko wa haraka katika masoko ya kimataifa.
Bei ya mafuta ghafi ilipanda kwa hadi asilimia 13 huku wawekezaji wakihamisha mitaji yao kutoka kwenye hisa na kuipeleka kwenye mali salama kama dhahabu na dhamana za serikali.
Bei ya mafuta aina ya Brent ilifikia dola 75.15 kwa pipa — kiwango cha juu zaidi katika kipindi cha miezi mitano. Hali hiyo inachochewa na hofu kwamba mashambulizi haya hayataishia hapa, huku Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiahidi kuendeleza operesheni hiyo mpaka "tishio hilo litakapoondolewa kabisa.”
Sekta za usafiri na burudani zaathirika vibaya
Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei amesisitiza kuwa Israel itarajie "adhabu kali” baada ya mashambulizi yake.
Katika masoko hisa za mabara ya Asia na Ulaya zilishuka mapema leo Ijumaa, huku masoko ya Marekani yakitarajiwa kufungua kwa hasara kubwa. Hisa za sekta ya nishati, na kampuni kubwa za ulinzi kama Lockheed Martin, Rheinmetall na BAE, zilipanda kwa wastani wa asilimia 2 hadi 3.
Sekta za usafiri na burudani zimeathirika vibaya, huku mashirika kadhaa ya ndege yakifuta safari zao kuelekea Mashariki ya Kati. Kufungwa kwa anga za Israel, Iran, Iraq na Jordan kumeongeza gharama za usafiri wa anga duniani.
Hali hii pia imeathiri sarafu ya Israel. Ijumaa, Shekel ya Israeli ilishuka kwa karibu asilimia 2 dhidi ya dola, baada ya serikali kutangaza "hali ya dharura.”
Katika miji mbalimbali, wananchi walimiminika madukani, hali iliyosababisha uhaba wa baadhi ya bidhaa, huku baadhi ya maduka yakiripoti ongezeko la wateja kwa asilimia 300.
"Kuongezeka kwa mvutano Mashariki ya Kati kumezidisha sintofahamu katika masoko ya fedha, huku wawekezaji wakiwa tayari na wasiwasi kuhusu sera za kibiashara za Trump. Bei ya mafuta ghafi ilipanda hadi asilimia 14 — ongezeko kubwa zaidi tangu uvamizi wa Urusi Ukraine — na hisa zikaporomoka duniani. Kadri mvutano unavyoendelea, dhahabu imeendelea kuimarika," alisema Carmel Crimmins, mtangazaji wa podcast ya reuters Econ World.
Kwa sasa, macho yote yameelekezwa kwenye Mlango wa Hormuz — uchochoro mwembamba wa bahari kati ya Iran, Umoja wa Falme za Kiarabu na Oman.
Takribani asilimia 20 ya mafuta yanayohitajika duniani hupitia kwenye mlango huo — sawa na mapipa milioni 18 hadi milioni 19 kwa siku. Iran imetishia mara kadhaa kuufunga mlango huo, hatua ambayo inaweza kufanya bei ya mafuta kupanda hata zaidi.
Athari zaidi kujitokeza mzozo ukitanuka
Iwapo mzozo huu utazidi kuongezeka, wachambuzi wanaonya kuwa usafirishaji wa bidhaa na nishati kutoka ukanda huo unaweza kukwama, na kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa dunia.
Barclays imeonya kuwa katika hali mbaya zaidi, mzozo unaweza kuathiri pia wazalishaji wengine wa mafuta na gesi katika ukanda huo na sekta ya usafirishaji kwa ujumla.
Athari zaidi zinaweza kuonekana iwapo mzozo huu utaenea hadi kwa makundi yanayioungwa mkono na Iran kama Hezbollah nchini Lebanon au Wahouthi nchini Yemen. Tayari mashambulizi ya meli za biashara katika Bahari ya Shamu mwaka jana yalisababisha ongezeko kubwa la gharama za usafirishaji.
Huku hayo yakiendelea, wachambuzi wa masuala ya fedha wanasema kuwa kuongezeka la bei ya mafuta kwa asilimia 10 pekee linaweza kuongeza mfumuko wa bei duniani kwa asilimia 0.4 ndani ya mwaka mmoja.
Hali hii inakuja wakati ambapo dunia bado inakabiliana na athari za vita vya Ukraine na sera za ushuru wa Marekani chini ya Rais Donald Trump, ambazo tayari zimevuruga biashara ya kimataifa.
Kwa sasa, wachumi wanaonya kuwa iwapo mzozo kati ya Israel na Iran utageuka kuwa vita ya muda mrefu, hatari ya mdororo wa uchumi wa dunia inaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.