IOM: Zaidi ya watu 40,000 wakimbia mashambulizi Cabo Delgado
4 Agosti 2025Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, limesema mashambulizi ya waasi kwenye mkoa wa Cabo Delgado kaskazini mwa Msumbiji yamesababisha zaidi ya watu 46,000 kuyahama makazi yao katika kipindi cha siku nane mwezi uliopita.
IOM limesema karibu asilimia 60 ya watu walilazimishwa kukimbia makazi yao ni watoto. Hata hivyo hakukuwa na taarifa za vifo katika mashambulizi hayo.
Katika ripoti nyingine, Ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa ilisema wimbi la mashambulizi kati ya Julai 20 na 28 katika wilaya tatu za Cabo Delgado lilisababisha kuongezeka kwa watu waliohama.
Umoja huo umewatuhumu wanamgambo wa jihadi kwa kuwakata vichwa wanavijiji na kuwateka watoto ambao wanawatumikisha kama vibarua au askari.
Kulingana na Umoja huo, vurugu, athari za ukame na vimbunga vilivyotokea miaka karibuni, vimesababisha zaidi ya watu milioni moja kuhama makazi yao kaskazini mwa Msumbiji.